Na Tiganya Vincent-RS-Tabora
Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la
Tabora limeitaka jamii pamoja katika kuungana katika kuwalinda
,kuwaheshimu na kusihi nao watu wenye ulemavu wa ngozi ili nao waweze
kutembea kifua mbele katika nchi hii kama walivyo watu wengine.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini
hapa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki mkoani Tabora Mhashamu Paulo
Luzoka wakati wa ufungaji wa mafunzo ya siku mbili juu ya kuwahudumia
watoto wenye ulemavu wa ngozi.
Alisema kuwa ni wajibu wa jamii
nzima bila kujali tofauti zake za kiimani kushirikiana na Serikali
katika kuhakikisha kuwa haki ya kuishi watu wenye ulemavu wa ngozi
inalindwa na kuwafanya waishi kwa amani na furaha.
Mhashamu Luzoka alisisitiza kuwa
ni vema jamii ikaweka nguvu katika kuelimisha jamii kuachana na vitendo
vya kikatili dhidi ya watu wenye ulemavu kwa imani za kishirikina
ambavyo vinawafanya watu hao wasiishi kama watoto yatima.
Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia
kuwafanya waishi bila hofu na hivyo kuwa huru katika kushiriki shughuli
mbalimbali za maendeleo katika maeneo yoyote ya nchi hii.
“Tusingependa kuona kuwa dawa ya
watu hao ikendelea kumwagika kwa sababu ya ulemavu wao…jifikie wewe
ungekuwa katika hali hiyo nawe ukatendewa kama wanavyofanyiwa watu hao
ungejisikiaje ? kama wewe unapenda kutendewa jambo jema basi mtende na
wewe albino jambo jema” alisema Askofu huyo wa Jimbo Kuu la Tabora.
Alisisitiza kuwa kama jamii
itaungana na kuishi kwa amani basi hakutakuwepo na mauaji ya watu wenye
ulemavu na wazee kwa sababu ya umri wao kuwa mkubwa na macho kubadilika.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Tabora
Aggrey Mwanri alilishukuru Kanisa kwa mpango wa kukabiliana na unyanyapa
kwa watoto wenye ulemavu katika jamii wakiwemo albino.
Alisema kuwa Serikali ya Mkoa wa
Tabora itasimama imara kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuwakata watu
wote wenye imani za kishirikina ambayo wamekuwa wakimwaga damu za watu
wenye ulemavu wa ngozi kwa mawazo ya kijinga kuwa watapata utajiri.
No comments:
Post a Comment