Mhe. Alli Karume Waziri wa Ujenzi,
Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
akipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na SSRA kutoka kwa
Afisa Uhusiano wa Mamlaka Bw. Sabato Kosuri alipotembelea banda hilo
wakati wa maadhimisho ya siku ya Bahari Duniani yaliyofanyika mkoani
Kigoma.
Na.Zawadi Msalla.
Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na
Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mh. Alli Karume ameitaka
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA)
kusimamia kwa ukaribu michango ya Wanachama kwenye Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii ili itumike kwa malengo yaliyokusudiwa kwa mujibu wa Sheria
zilizoanzisha mifuko hiyo.
Wito huo umetolewa jana mjini
Kigoma na Waziri Karume alipotembelea banda la SSRA kwenye maonesho ya
wiki ya Bahari duniani yanayoendelea kwenye viwanja vya shule ya msingi
Mlole Mkoani humo.
Waziri Karume alisema SSRA
inawajibu mkubwa wa kumlinda mwanachama wake ili kuhakikisha hapati
matatizo pale anapotakiwa kupata mafao yake.Pia alisisitiza kuwa Itakuwa
ni jambo la kuumiza sana inapotokea mwanachama mwenye matumaini ya
kupata mafao yake atakapoambiwa mfuko umefilisika na hivyo mafao
anayoyatarajia hawezi kuyapata.
Aidha Mhe. Karume aliipongeza SSRA
kwa elimu wanayoendelea kuitoa kwa jamii juu ya umuhimu wa kujiunga na
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na jinsi wanavyo simamia maboresho
mbalimbali yanayoendelea katika sekta hiyo.
Hata hivyo alisema bado SSRA
inawajibu mkubwa wa kutoa elimu kwa jamii ili kushawishi wananchi kuona
umuhimu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwani wapo wananchi wengi wasio
fahamu umuhimu wa mifuko hiyo na wengi wao hupata shida inapofikia
kipindi cha uzeeni.
Awali akitoa maelezo ya shughuli
za SSRA Afisa Uhusiano na Uhamasishaji wa Mamlaka hiyo Bw. Sabato
Kosuri alimhakikishia Mhe. Waziri usalama wa michango ya wanachama
kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Bw.Kosuri alisema tayari SSRA
imeweka miundombinu imara ya kusimamia eneo hilo ikiwa ni pamoja na
miongozo ya uwekezaji pamoja na kaguzi za mara kwa mara ili kuhakikisha
mifuko inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria kanuni na taratibu na hivyo
kuwahakikishia usalama wachangiaji wote kwenye mifuko ya hifadhi ya
jamii.
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti
wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii iliundwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi
wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135 (Toleo la 2015) kwa lengo la
kusimamia na kudhibiti Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa manufaa ya
Wanachama na Taifa kwa ujumla. Mamlaka ilianza kazi rasmi mwishoni mwa
Mwaka 2010.
Mamlaka ina jukumu la msingi
la kuhakikisha kwamba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inakuwa endelevu,
inaendeshwa kwa kufuata kanuni, taratibu na kisheria, wanachama wanapata
taarifa za Mifuko/michango yao, na mafao yaliyobora.
No comments:
Post a Comment