Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi (wa pili kulia)
akioneshwa Mfumo wa kukusanya Mapato wa Kielektroniki uliopo Kituo cha
Taifa cha Data, Dar es Salaam na mtaalamu wa umeme na mifumo ya upozaji
wa Kituo hicho Bwana. Deus Lwabukuna.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi (aliyesimama)
akifafanua jambo kuhusu utayari wa taasisi za Serikali yake kutumia
Kituo cha Taifa cha Data kilichopo Dar es Salaam. Anayesikiliza wa
kwanza kushoto ni Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Dkt. Eng. Maria Sasabo na wa kwanza kulia ni Mtendaji
Mkuu wa TTCL Bwana Waziri Waziri Kindamba.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Moshi Kakoso (aliyesimama) akichangia
jambo kuhusu matumizi ya Kituo cha Taifa cha Data wakati wa ziara ya
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Balozi
Seif Ali Iddi (hayupo pichani) alipotembelea kituo hicho Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya
Simu Tanzania (TTCL) Eng. Omary Nundu (aliyesimama) akisisitiza jambo
wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi (hayupo pichani) alipotembelea kituo
cha Taifa cha Data kilichopo Dar es Salaam.
Muonekano wa Mfumo wa Kukusanya
Mapato wa Kielektroniki (electronic Revenue Collections System – eRCS)
uliopo kwenye Kituo cha Taifa cha Data kilichopo Dar es Salaam.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imevutiwa na utendaji kazi wa Kituo cha Taifa cha Data (National
Internet Data Centre-NIDC) kwa kukusanya mapato ya Serikali kwa kutumia
Mfumo wa Kukusanya Mapato wa Kieletroniki (eRCS – electronic Revenue
Collections System)hivyo kuongeza mapato ya Serikali ya Muungano ya
Tanzania na Mapinduzi ya Zanzibar.
Hayo yameelezwa leo na Makamu wa
Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali
Iddi alipotembelea Kituo cha Taifa cha Data kilichopo Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Balozi Iddi amevutiwa na kuridhishwa na utendaji kazi
wa Kituo hicho ambapo kinatumia Mfumo wa Kukusanya Mapato wa
Kielektroniki ambao umeunganisha taasisi za Serikali na sekta binafsi.
“Zanzibar tunategemea sekta ya utalii kuongeza mapato yetu, wadau wote
wa sekta hii wajiunge na mfumo huu pamoja na taasisi zote za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ili tuweze kuona makusanyo ya mapato yetu kwa
wakati, ufanisi na kwa uhakika”, amesema Balozi Iddi. Mhe. Balozi Iddi
ameongeza kuwa Mfumo huu unasaidia kukusanya mapato ya Serikali,
Serikali inataka kuwatumikia wananchi wake na kuwaletea maendeleo na
hakuna Serikali yoyote inayoweza kufanya hayo bila ya kodi.
Katibu Mkuu wa Mawasiliano, Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Eng. Maria Sasabo ambaye
amemuwakilisha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame
Mbarawa amesema kuwa Serikali ya Muungano wa Tanzania tayari
inashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mfumo huu
kukusanya na kuongeza mapato ya Serikali ambapo yatawezesha Serikali
zetu kuhudumia wananchi wake katika nyanja ya afya, elimu, miundombinu,
maji, barabara na kilimo cha kisasa.
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu
Tanzania (TTCL) Bwana Waziri Waziri Kindamba amesema kuwa Mfumo huo
umetengenezwa na wataalamu wazalendo wa watanzania wakishirikiana kwa
pamoja kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na wanahusika katika uendeshaji wa Mfumo huo.
Pia, ameongeza kuwa taasisi za Serikali na sekta binafsi zitumia Mfumo
huo na hadi hivi sasa jumla ya Kampuni saba za mawasiliano na benki kumi
na nne zimeunganishwa kwenye Mfumo huo na makusanyo ya mapato yao
yanapita na kuonekana kwenye Mfumo huo. Bwana Kindamba amesema kuwa
Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imeweza
kuongeza makusanyo ya mapato yake kutoka shilingi milioni kumi na tatu
hadi milioni mia tano kwa mwezi kupitia Mfumo huo tangu ulipoanza rasmi
kutumika ulipozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
John Pombe Magufuli mwezi Juni mwaka huu hadi Agosti mwaka huu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Moshi Kakoso ameiomba Kampuni ya
Simu Tanzania (TTCL) kufanya kazi kibiashara zaidi na kwa faida na sio
kwa mazoea kama hapo awali. Vile vile Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Eng.
Omary Nundu amesema kuwa azma ya Bodi yake ni kuhakikisha kuwa TTCL
inaendelea kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi nchi nzima na
ameiomba Serikali kuendelea kuiunga mkono kampuni kongwe ya kizalendo,
TTCL ili iweze kujiendesha kwa faida.
Kituo cha Taifa cha Data
kimejengwa na Serikali ya Muungano ya Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano kuanzia mwaka 2014 na kukamilika mwaka 2015 kwa
gharama ya dola za marekani milioni thelathini na tano na ni cha
kiwango cha kimataifa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment