Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametoa wito wa kutafakari upya
mtazamo wa serikali ya Ujerumani kuelekea Uturuki baada ya nchi
hiyo kuwakamata raia wawili zaidi wa Ujerumani.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeporomoka tangu jaribio lililoshindwa la mapinduzi mwaka 2016.
Hakuna "msingi wa kisheria" wa kukamatwa katika matukio mengi, Merkel
amesema , akielezea kuhusu Wajerumani wawili waliokamatwa siku ya
Alhamis nchini Uturuki, na kufikisha jumla ya idadi ya raia wa
Ujerumani waliokamatwa nchini humo kwa sababu za kisiasa kuwa 12.
"Hii ndio sababu tunahitaji kuchukua hatua muhimu hapa," amesema ,
na kuongeza kwamba serikali "huenda inapaswa kutafakari upya"
uhusiano wake na Uturuki.
Merkel amesema Ujerumani tayari, "imeendeleza kwa kiasi kikubwa "
uhusiano wake na Uturuki, lakini hatua hii mpya ina maana "huenda
ni muhimu kutafakari upya zaidi," na kuongeza kwamba kunaweza
kuwa na mazungumzo zaidi juu ya ushiriki wa Ankara katika Umoja
wa forodha wa Umoja wa Ulaya hadi pale hali ya hivi sasa
itakapotatuliwa.
"Madai yetu kwa Uturuki yako wazi kabisa," msemaji wa serikali ya
Ujerumani Steffen Seibert amesema. "Tunatarajia Uturuki itawaachia
huru raia wa Ujerumani ambao wamekamatwa kwa misingi isiyokuwa ya
kisheria."
Mahusiano baina ya washirika hao wa NATO yamevurugika tangu pale
serikali ya Ujerumani ilipoikosoa Uturuki kuhusiana na
ukandamizaji uliofuatia jaribio la mwaka jana lililoshindwa la
mapinduzi.
Kukamatwa Wajerumani
Kukamatwa kwa Wajerumani wawili siku ya Alhamis kunafikisha idadi
ya watu 55, Wajerumani waliokamatwa nchini Uturuki, 12 kati yao
wanashikiliwa kwa sababu za kisiasa na wengine wanne wana uraia
pacha wa Ujerumani na Uturuki , ikiwa ni pamoja na mwandishi
habari mwenye uraia wa Uturuki na Ujerumani Deniz Yucel, ambaye
yuko kizuwizini sasa kwa siku 200, imesema wizara ya mambo ya
kigeni ya Ujerumani.
Shirika la habari la Uturuki linaloendeshwa na serikali Anadolu
limeripoti kwamba raia wawili wa Ujerumani wenye asili ya
Uturuki wamekamatwa katika uwanja wa ndege wa Antalia kwa madai
ya kuwa na uhusiano na mtandao wa imamu anayeishi uhamishoni
nchini Marekani Fethullah Gulen , ambaye Ankara inamshutumu kwa
kutayarisha jaribio la mapinduzi lililoshindwa mwaka jana.
Kiongozi wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan
Ujerumani haijafahamishwa rasmi kuhusiana na kukamatwa kwa watu
hao wawili, ambako kulitokea katika uwanja wa ndege wa Antalia
siku ya Alhamis.
Ubalozi mdogo wa Ujerumani katika mji wa pwani wa Izmir
ulifahamishwa kuhusu kukamatwa huko "na vyanzo ambavyo si vya
serikali," msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Maria Adebahr
aliwaambia waandishi habari.
"Tunajaribu kujua wanashitakiwa kwa madai gani," amesema Adebahr.
"Tunapaswa kufikiria kwamba ni madai ya kisiasa, shaka ya ugaidi,
kama ilivyo kwa wengine."
Wanadiplomasia hawajaweza kuwa na mawasiliano nao , ameongeza,
sikukuu ya Ijumaa ya Kiislamu ya Eid al-Adha ikiwa ni sababu
mojawapo ya uchelewesho wa mawasiliano na maafisa.
No comments:
Post a Comment