JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara yake ya kwanza nje ya
nchi leo tarehe 06 April, 2016 kwa kutembelea nchi jirani ya Rwanda,
ambapo yeye na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mheshimiwa Paul
Kagame wamefungua Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani (One
Stop Border Post) na Daraja la Kimataifa la Mto Rusumo katika Mpaka wa
Tanzania na Rwanda.
Rais Magufuli ambaye ameongozana
na Mkewe Mama Janeth Magufuli, ameingia nchini Rwanda kwa usafiri wa
magari akitokea nyumbani kwake Lubambangwe, katika kijiji cha Mlimani,
Wilaya ya Chato Mkoani Geita ambako alikuwa mapumziko tangu tarehe 29
Machi, 2016
Katika eneo la Rusumo, Rais
Magufuli na Rais Kagame kwanza wamefungua majengo ya Kituo cha Pamoja
cha Utoaji wa Huduma za Mpakani kilichopo upande wa Tanzania, kisha
wakafungua daraja la mto Rusumo, na baadaye wakafungua Majengo ya Kituo
cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpakani kilichopo upande wa Rwanda.
Mradi huu wa ujenzi wa Kituo cha
Pamoja cha utoaji wa Huduma za Mpakani cha Rusumo, umehusisha ujenzi wa
majengo ya mamlaka ya Mapato katika pande zote mbili na daraja lenye
urefu wa mita 80 na upana wa mita 9.5, na umegharimu shilingi Bilioni
61.4 zilizotolewa kwa ufadhili wa serikali ya Japan kupitia shirika lake
la JICA.
Akizungumza katika sherehe ya
ufunguzi wa mradi huo Rais Magufuli ameishukuru Japan kwa kutoa fedha za
kuwezesha utekelezaji wa mradi huo na ametoa wito kwa wafanyabiashara
wa Rwanda kupitisha mizigo yao Tanzania kupitia mpaka huo, pamoja na
kuitumia bandari ya Dar es salaam.
Dkt. Magufuli amewasihi wananchi
wa Rwanda na wanajumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla, kushirikiana
kibiashara kwa kutumia fursa zilizopo huku akibainisha kuwa Tanzania
imeanza juhudi za kuimarisha miundombinu yake ya barabara na kujenga
reli ya kati, ambayo tayari washirika 13 wameonesha nia ya kufanikisha
ujenzi huo.
Aidha, Rais Magufuli amewaonya
maafisa forodha na vituo vya ukaguzi kuacha mara moja tabia ya
ucheleweshaji wa upitishaji wa mizigo, na amesema serikali imeshaamua
kuwa barabara ya Rusumo hadi Dar es salaam itakuwa na vituo vitatu
ambavyo ni Rusahunga, Singida na Vigwaza ili magari yatumie muda wa siku
3 badala ya kutumia siku zaidi ya 10
Kwa upande wake Rais Paul Kagame
wa Rwanda ambaye ameongozana na mkewe Mama Janeth Kagame, pamoja na
kuishukuru Japan kwa kufadhili mradi huo amesema Tanzania na Rwanda zina
kila sababu ya kushirikiana kiuchumi na ameongeza kuwa ni matumaini
yake kujengwa kituo hicho kutaongeza biashara na idadi ya watu wanaovuka
daraja kutoka 2,000 wa sasa hadi watu zaidi ya 15,000 kwa siku.
Akiwa Rwanda Rais, Magufuli
amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Paul Kagame na hapo Kesho Rais
Magufuli atashiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 22 ya mauaji wa
Kimbari yaliyotokea mwaka 1994 ambapo watu takribani milioni 1,000,000
waliuawa.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Kigali
06 April, 2016
No comments:
Post a Comment