Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, Ameunda
Kamati ya mpito ya kusimamia uanzishwaji wa Tume ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo ameipa miezi sita kufanya kazi kuanzia
mwezi Aprili, 2016 ya kuhakikisha kuwa Tume ya TEHAMA inaanza kazi
rasmi.
Katika
kuhakikisha kuwa Tume ya TEHAMA inaanza kazi mara moja, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya
Mawasiliano, Prof. Faustin Kamuzora, amewakabidhi wajumbe wa Kamati hiyo
Amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Na.532 iliyotolewa
kupitia gazeti la Serikali Na. 47 la tarehe 20 Novemba, mwaka 2015
iliyoanzisha Tume na Hadidu za Rejea zinazoainisha majukumu yao.
Majukumu
hayo ni pamoja na kusimamia uanzishwaji wa Tume, kuandaa sheria ya
kuanzisha Tume, na kutengeneza Mpango Mkakati wa Tume.
Prof.
Kamuzora amewataka wajumbe wa Tume hiyo kuepuka kuweka mitazamo au
maslahi binafsi ya wao wenyewe au ya taasisi zao katika kipindi cha
kuanzisha Tume, bali waishauri Serikali namna nzuri ya kuhakikisha kuwa
Tume hiyo inaanza kazi ya kusimamia na kuratibu masuala ya TEHAMA
nchini.
Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wao na Katibu wa Kamati ya Kuanzisha Tume ya TEHAMA nchini ni kama ifuatavyo:
- James Kilaba (Mwenyekiti), Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,
- Samson Mwela (Katibu), Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
- Idris Rai (Mjumbe), Makamu Mkuu wa Chuo, SUZA,
- Joan Mbuya (Mjumbe), Mkurugenzi wa Sera na Mipango-Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali,
- George Mulamula (Mjumbe), Mkurugenzi Mtendaji-DTBi,
- Juma Rajabu, (Mjumbe), Mkurugenzi Mtendaji-Maxcom Africa,
- Maharage Chande, (Mjumbe), Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Ofisi ya Rais-President’s Delivery Bureau, na
- Nicolaus Mhonyiwa (Mjumbe), Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA-Ofisi ya Msajili wa HAZINA.
Aidha,
Tume ya TEHAMA inatarajiwa kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwa ni
pamoja na yafuatayo: Kushiriki katika kushauri juu ya uwekezaji wa
TEHAMA nchini kwa ubia na sekta binafsi; kuwatambua, kujenga uwezo na
kuwaendeleza wataalam wa TEHAMA; kushauri na kushiriki pamoja na wadau
katika tafiti za TEHAMA, uwekaji viwango na ubunifu katika sekta ya
TEHAMA; na kushiriki katika kusimamia miundombinu na programu za kitaifa
za TEHAMA.
Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
anayeshughulikia Mawasiliano, Dkt. Eng. Maria Sasabo, alisisitiza kuwa
Kamati ina kazi kubwa ya kuona namna bora zaidi ya kuhakikisha kuwa Tume
itatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na masuala ya
uwekezaji; na kusimamia vema viwango vya wataalamu wa Sekta. Naye
Mwenyekiti, Inj. James Kilaba, kwa niaba ya Kamati alishukuru kwa
kuaminiwa na Serikali na pia aliahidi kuwa watatekeleza majukumu yao
kikamilifu. Pia alimalizia kwa kusema, “hatutawaangusha”.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikali
No comments:
Post a Comment