Waandishi wa habari wakifatilia kwa makini maelezo ya
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi Kamishina Diwani Athuman
hayupo pichani wakati wa mkutano wa kuelezea mikakati na Malengo ya
Serikali katika kupamabana na kudhibiti wahalifu wa kuhujumu uchumi
uliofanyika leo jijini Dar es salaam.
Na Kalonga Kasati
Serikali inaendelea kusimamia
urejeshaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya kihalifu kupitia mpango
wa kupambana na uhalifu ulioanzishwa mwaka 2012 kwa kuwashtaki na
kuwataifishia mali zao pindi upelelezi ukikamilika na kubainika mhalifu
ana makosa hayo.
Baadhi ya watuhumiwa kadhaa wamepelewa mahakamani na kufungwa, ikiwemo mali zao kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi
wa Mashtaka nchini ( DPP) Biswalo Mganga wakati wa Mkutano wake na
waandishi wa habari uliofanyika leo kwenye ofiisi za Makao Makuu ya
Jeshi la Polisi jijini Dar es salaam, ambapo alisema kuwa hatua hizo
zimechukuliwa mara baada ya upelelezi wa makosa ya kuhujumu uchumi
kukamilika na kumbaini mhusika.
Aidha Mganga
aliongeza kwamba mhusika hushtakiwa na mali zake kutaifishwa kulingana
na kosa lake, pia suala hili litamgusa kila mtu, wakiwemo watumishi wa
umma.
“Mhalifu wa kuhujumu uchumi wa
nchi ikiwemo usafirishaji wa nyara za Serikali, uuzaji wa madawa ya
kulevya na kujipatia mali kwa njia ya rushwa watatumikia adhabu ya
kulipa faini, kufungwa jela na kutaifishiwa mali zake pindi atapobainika
na makosa hayo” alisema Mganga.
Alisema kufuatia mkakati huo,
Jeshi la Polisi limekamilisha upelelezi wa kesi 23 ambazo ziliwasilishwa
kwa DPP na kati ya hizo tatu (3) zimetolewa uamuzi na nyingine ishirini
(20) ziko katika hatua ya maombi ya kupata amri ya mahakama ili ziweze
kuziwa au kutaifishwa.
Alizitaja baadhi ya kesi za dawa za kulevya ambazo zimefikia ukomo na kutolewa uamuzi Januari 27, mwaka huu.
Mkoani Kilimanjaro kesi
mojawapo ni Josephine Waizela, ambaye ni raia wa Kenya aliyetiwa hatiani
kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya Cocaine zenye uzito wa
kilogram tatu zikiwa na thamani ya Sh. Milioni 162 na kufungwa kifungo
cha maisha.
Kesi nyingine ni namba 46 ya
mwaka 2014 kutoka pia mkoani Kilimanjaro ambayo ilihusisha watu watatu,
mmoja kati yao ambaye ni Hamis Mbwana alitiwa hatiani kwa kukutwa na
dawa za kulevya aina Heroine zenye uzito wa gram 3191.11 na thamani ya
Sh. Milioni 143, watuhumiwa wengine wawili katika kesi hiyo waliachiwa
huru.
Mganga alizitaja baadhi ya kesi
nyingine za uhujumu uchumi ni namba 6 ya mwaka 2015, ilisikilizwa
mkoani Mbeya ambayo iliwahusisha raia wanne kutoka nchini China
waliotiwa hatiani kwa kosa la kukutwa meno ya vifaru 11. Raia hao ni
Song Lei , Xiao Shaodan, Chen Jianlin na HU Liang, ambao wamehukumiwa
kifungo cha miaka 20 na kulipa faini ya Sh. Milioni 9,288 kwa kila
mmoja.
Kesi nyingine ya uhujumu
uchumi namba 3 ya mwaka 2016 iliyomhusisha raia wa Tanzania Amani Rashid
Ngaza aliyetiwa hatiani kwa kosa la kukutwa na meno ya tembo nane
iliyosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Katavi, wilaya ya
Mpanda. Mtuhumiwa huyo amefungwa kifungo cha miaka 30 na kullipa faini
ya Sh. bilioni 1.2.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi
Maganga alibainisha baadhi ya mali zilizotaifishwa kutoka kwa wananchi
kuwa ni magari matano aina ya Toyota Rv 4 mbili ,Suzuki, Toyota Surf ,
Hiace pamoja na nyumba kutoka kwa washtakiwa mbalimbali wa makosa ya
kuhujumu uchumi.
Aidha, Mganga alitoa rai kwa
wananchi kutoa ushirikiano bila uwoga katika kufichua mali za mafisadi
ili sheria ichukue mkondo wake pamoja na kuwataka wananchi wasijihusishe
kwa njia yoyote ile ili kuficha umiliki wa mali ya mtu mwingine
aliyoipata kiharamu kwa nia ya kuficha uhalifu wake kwani kufanya hivyo
ni kosa kisheria.
“Kwa mujibu wa Sheria aliyeshirikikuficha mali ya mtu
mwingine inayohusiana na uhalifukwa njia yoyote ile pia anaweza
kushitakiwa kama aliyetenda kosa la ufisadi,” alisema.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Jeshi la Polisi Kamishna Diwani Athumani alisema kuwa
atakayekamatwa na kosa la wizi au mali ya haramu atatumikia adhabu na
mali zake kutaifishwa.
“Mhalifu akibainika na mshataka
ya wizi au kujipatia mali kwa njia ya haramu atatumikia adhabu na
kutaifishiwa mali zake kama vile magari, nyumba, boti, viwanja na fedha
taslimu” alisema Kamishna Athumani.
Aidha, Kamishna Athumani
aliongeza kuwa uzoefu wao unawaonyesha kwamba wahalifu wanatumia majina
ya wake zao, waume zao, watoto wao na wakati mwingine kutumia majina ya
watu ambao hawapo ili kuendelea kufaidika na mali walizozipata kwa niia
za uhalifu.
“Hakuna mhalifu atakayepona katika mapambano haya pia uhalifu haulipi na hauna nafasi nchini” alisistiza Kamishina Athuman.
Mbali na hayo, Mkurugenzi wa
upelelezi Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU) Alex
Mfungo pia alisema kuwa wameanzisha kitengo cha kutaifisha mali
zilizopatikana kwa njia ya uhalifu ikiwemo rushwa.
Tangu mwaka 1990, Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitambua utaifishaji wa mali
zilizopatikana kwa njia ya kihalifu kama kipaumbele katika mfumo wa haki
jinai wa kupigana na uhalifu. Haisadii sana katika jitihada za
kupambana na uhalifu ikiwa mhalifu atapata adhabu ama ya kutozwa faini
au kwenda jela ikiwa ataachiwa uhuru na kupewa fursa ya kutumia fedha au
mali iliyopatikana kwa uhalifu huo.
Zaidi, fedha zilizoibwa na
wanasiasa wala rushwa pamoja na wahalifu wengine, zinahitaji kutaifishwa
na kuelekezwa katika maeneo muhimu yenye mahitaji.
Sheria ya Utaifishaji wa Mali
Haramu ilipitishwa na Bunge mwaka 1991 ili kuendana na muelekeo wa
Kimataifa pamoja na mikataba ya Kimataifa ambayo imeridhiwa na nchi
yetu.
No comments:
Post a Comment