Thursday, 14 January 2016

BIA3Na Kalonga Kasati
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akifungua mkutano wa miradi ya ubia katika ujenzi  wa Miundombinu kati ya Japan na Tanzania kwenye hoteli ya Hyatt Regency- Kilimanjaro jijini Dar es salaam Januari 14,2016.
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka watanzania  kujikita katika kuimarisha Miundombinu  ili kukuza uchumi, kuimarika kwa miundombinu ya usafirishaji ni muhimu kwa shughuli mbalimbali mfano kilimo na biashara.
Akizungumza  na  wadau wakati akifungua  mkutano wa Miradi ya Ubia katika Ujenzi wa Miundombinu kati ya  Tanzania na Japan(TANZANIA -JAPAN PUBLIC -PRIVATE QUALITY INFRASTRURE CONFERENCE) uliofanyika leo,  katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, amesema  sekta   binafsi  inasaidia katika ujenzi wa Miundombinu  na sekta ya usafirishaji kwa ujumla, ambapo ni muhimu kwa vile inasaidia kuboresha maisha ya watu.
“Serikali kupitia Kituo cha uwekezaji nchini (TIC) imeandaa mazingira mazuri ya Biashara inayosaidia wawekezaji kuja kuwekeza nchi,
 Matumaini yetu ni kwamba kutokana na mkutano huu   wawekezaji wa ndani  mtapata  fursa ya kujifunza na kujiunga katika  
kampuni ambazo zitawasaidia  kushirikiana na kampuni za kijapani  na kuweza kupata ujuzi,  utaalamu wa kiutawala na uwezo wa 
kuwa wabunifu zaidi hasa katika masuala ya miundombinu.”  amesema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Majaliwa ameendelea kwa kusema mkutano huu utaimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japani, na kutoa fursa ya kubadilishana ujuzi kwa wakandarasi, washauri, kampuni za biashara na uhandisi kutoka Japani na Tanzania, vilevile utawawezesha kujenga mtandao kwa kushirikiana na makampuni ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wa  miundombinu na usafirishaji,  Tanzania ina ukubwa wa barabara zinazofikia kilomita 87,581, kutokana na sera na jitihada mbalimbali  kwa  kipindi cha miaka 10 (2005-2015) jumla ya kilomita 17,762  zimefikia hatua mbalimbali za ujenzi.
Waziri Mkuu ameendelea kwa kusema, Tanzania ina mifumo miwili ya reli, reli ya kati yenye kilomita 2,706 na reli ya ‘Tanzania Zambia Railway Authority’ (TAZARA) yenye kilomita 975. Pia, ina Bandari kuu za Dar es salaam, Tanga na  Mtwara .
Kwa upande wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kupitia  Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa (National ICT Broadband Backbone -NICTBB)  kwa kutumia mfumo wa baharini (SEACOM, July 2009) na (EASSY April,2010)  tayari nchi jirani za Rwanda, Zambia na Kenya zimeunganishwa na mkongo huo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani, amesema miundombinu ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya nchi yeyote ile duniani. Tanzania na Japani zimeshirikiana katika ujenzi na uboreshaji Wa miundombinu mbalimbali, mfano barabara za Dodoma –Iringa, Namtumbo –Tunduru, Dodoma – Babati  inayoendelea  kujengwa, upanuzi wa barabara ya Gerezani  pamoja na   ‘fly over’ ya TAZARA.
Naye, Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Uchukuzi na Utalii wa Japani Takatoshi Nishiwake amesema, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda alipotembelelea Japani Alisema angependa kuona Japani na Tanzania zinashirikiana katika masuala ya ujenzi wa miundombinu.
 Ameendelea kwa kusema kuwa, Serikali ya Japani inapenda kubadilishana ujuzi na Tanzania katika masuala ya miundombinu, pia ni matumaini yake kuwa washiriki kutoka pande zote mbili wanapata fursa ya kubadilishana ujuzi na kujifunza zaidi. Vile vile kupitia mkutano huu mahusiano ya nchi hizi mbili yataimarika zaidi.

No comments:

Post a Comment