Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa George B. Simbachawene
(Mb) amewasimamisha kazi Wakurugenzi Watendaji wa Manispaa za Kigoma,
Mkoa wa Kigoma na Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi kwa tuhuma za
kuridhia na kutekeleza maamuzi ambayo yamesababishia Serikali hasara na
upotevu wa fedha.
Mkurugenzi Wa Manispaa ya Kigoma
Mhandisi Boniface Nyambele anakabiliwa na tuhuma ya Uuzaji wa Nyumba za
Halmashauri bila kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo na bila
kibali cha Waziri Mwenye Dhamana kama Sheria inavyo elekeza.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda
Ndugu Suleiman Lukanga ana kabiliwa na tuhuma za Ununuzi hewa wa gari la
kusomba taka kwa kiasi cha shilingi milioni tisini na mbili na laki Saba na elfu hamsini (92,750,000/=) na ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa
Skimu ya Umwagiliaji ya Kakese kiasi cha shilingi milioni mia mbili,
tisini na nne (294,000,000/=).
Aidha, Mheshimiwa Waziri wa Nchi
ameagiza nafasi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma ikaimiwe na Mhandisi
Sultan Imari Ndilowa ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maji, Manispaa ya
Kigoma, nafasi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda ikaimiwe na Ndugu
Lauteri John Kanoni ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi kutoka Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Waziri wa Nchi,
amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote
Nchini kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao wafuate Sheria,
Kanuni na Taratibu zilizopo. Serikali haitasita kuchukua hatua za
kinidhamu kwa watumishi wote ambao watakiuka matakwa ya Sheria, Kanuni
na Taratibu na kutoweka mbele maslahi ya Umma.
No comments:
Post a Comment