Na Kalonga Kasati
Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini Mhe.Jaji Francis Mutungi ameviasa Vyama vya Siasa kushiriki
chaguzi zinazotangazwa na tume za uchaguzi nchini ikiwemo uchaguzi wa
Machi 20, mwaka 2016 uliotangzwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Kwa mujibu wa barua
iliyotolewa kwa vyama hivyo leo na kusainiwa na Jaji Mutungi ilieleza
kwamba, kimsingi Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258 inasisitiza
vyama vya siasa kushiriki katika chaguzi zote zinazotangazwa na tume za
uchaguzi ili kufikia malengo yake ya kushika dola.
“Katika nchi kidemokrasia na
kwa chama cha siasa kinachoamini misingi ya kidemorasia ya vyama vingi
vya siasa, hakuna njia mbadala kwa chama cha siasa kufikia malengo yake
zaidi ya kushiriki uchaguzi.
“Ni wajibu wa kila chama cha
siasa nchini kama wakala wa kukuza demokrasia, utawala wa sheria na
amani ya nchi, kuwa wa kwanza kutii matamko ya kisheria yanayotolewa na
mamlaka husika . Kama kuna chama cha siasa hakiridhiki au kimekwazwa kwa
njia moja au nyingine na suala lolote kuhusu masuala ya uchaguzi, njia
stahiki na inayonyesha ukomavu wa kisiasa si kuhamasisha kugomea
uchaguzi, bali ni vema kikafuata utaratibu uliowekwa katika sheria za
uchaguzi,” alisema Jaji Mutungi.
Aidha Msajili huyo amesema kwa
mujibu wa Sheria za Nchi bado ni suala la hiari kwa chama kushiriki
uchaguzi lakini utashi huo wa hiari unaenda sanjari na umuhimu wa kila
chama kushiriki kila uchaguzi unaotangazwa na tume ya uchaguzi.
“Hivyo ni muhimu basi kila
chama cha siasa kuelewa kuwa,uchaguzi ni kipimo cha uhai wa chama cha
siasa. Chama cha siasa kisiposhiriki uchaguzi kinaua uhai wake katika
mtazamo wa harakati za kisiasa,” alisisitiza.
Aliongeza kwamba hivi sasa,
mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na vyama vya siasa vimeimarika, hivyo
sio vyema kwa chama cha siasa kujirudisha nyuma au kujiua kisiasa kwa
kutoshiriki uchaguzi wakati kina uwezo wa kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment