Na Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amesema Serikali imepanga kufungua viwanda vya kusindika Ngozi kwenye
mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam ili kutoa soko kwa ngozi za
wanyama wanaochinjwa kwenye machinjio ya mikoa hiyo.
Ametoa kauli hiyo jana jioni
(Jumatatu, Januari 18, 2016) wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania
waishio Botswana kwenye kikao kilichofanyika kwenye kituo cha mikutano
ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Waziri Mkuu alikuwa nchini
Botswana kwa ziara ya siku moja kumwakilisha Rais Dk. John Pombe
Magufuli kwenye mkutano wa SADC Double Troika yaani kikao maalum cha
Wakuu wa Nchi na Serikali (SADC Summit) na Wakuu wa Nchi wanaounda
Chombo cha Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi Na Usalama (SADC Organ on
Politics, Defense and Security Cooperation) uliofanyika kwenye kituo cha
mikutano ya kimataifa (GICC), jijini Gaborone, Botswana.
Akizingumza na Watanzania hao,
Waziri Mkuu alisema: “Tumeamua kufungua viwanda vya kusindika ngozi
kwenye mikoa ya Shinyanga, Geita na Dar es Salaam (kule Pugu) ili ngozi
zikishachunwa, zipelekwe moja kwa moja kiwandani,” alisema.
Alisema Serikali imeamua kuongeza
viwanda nchini kama njia mojawapo ya kukuza uchumi, kuacha kuuza mali
ghafi lakini pia ni fursa ya kuongeza ajira kwa Watanzania.
Akijibu hoja zilizoainishwa
kwenye risala yao, Waziri Mkuu alisema Serikali bado ina nia ya kuhamia
Dodoma na kwamba itaendelea kutenga fedha zaidi ili wizara nyingi
zijenge ofisi zao Dodoma. “Serikali ilikwishaamua kwamba Dodoma ni mji
wa kiserikali na Dar es Salaam ni mji wa kibiashara. Kwa sasa kuna
baadhi ya Wizara zimeshajenga ofisi Dodoma na kuna taasisi kama vile
Benki Kuu nazo pia zimejenga ofisi zake Dodoma. Tutaendelea kutenga
fedha zaidi ili wizara nyingine zikamilishe ujenzi wa ofisi zao,”
alisema.\
Waziri Mkuu Majaliwa alitumia
fursa hiyo kuwataka Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) Watafute
fedha za mitaji ama zao ama kupitia kwa marafiki zao ili waweze kuwekeza
nyumbani (Tanzania).
“Nia ya Serikali sasa hivi ni
kufungua milango kwa wawekezaji hasa wenye nia ya kujenga Viwanda.
Njooni nyumbani muone ni eneo gani mnaweza kuwekeza, kama mna miradi
huku Fungueni matawi kule nyumbani. Serikali inajivunia uwepo wenu kwa
sababu inatambua kwamba Huku mliko kuna kitu mnajifunza na mnaweza
kukirudisha nyumbani kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla,”
alisema.
Mapema, akisoma risala yao kwa
niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha Watanzania Waishio nchini
Botswana (The Association of Tanzanians in Botswana – ATB), Bw. Neiman
Kissasi alisema chama hicho kilianzishwa mwaka 1992 kikiwa na lengo la
kuwaunganisha Watanzania waishio Botswana pamoja kujenga undugu wao na
kusaidiana.
Katika risala yao, walishauri
wafugaji wa Tanzania waelimishwe na kuwezeshwa kufuga kisasa na
kuondokana na ufugaji wa kurandaranda. Pia waliiomba Serikali iongeze
kasi ya mpango wake wa kuhamisha shughuli zote za Serikali mjini Dodoma,
kwani itasaidia kupunguza matumizi ya Serikali kwa kuwa shughuli za
Serikali zitakuwa zinafanyika eneo moja.
Vilevile, waliiomba Serikali
ifungue fursa za kiuchumi kwenye mikoa mingine ya Tanga, Lindi, Mtwara,
Pwani, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Arusha badala ya kuziacha ziwe Dar es
Salaam peke yake. “Hii itasaidia kuibua fursa za kiuchumi na kupunguza
msongamano katika Jiji la Dar es Salaam”, ilisema sehemu ya risala yao.
No comments:
Post a Comment