Waziri Mkuu wa Lesotho Pakalitha Mosisili amepigiwa kura ya kutokua na imani naye na bunge la nchi.
Kufuatia hatu hio, bunge la taifa litavunjwa na uchaguzi mwingine kufanyika.
Hii ndio mara ya pili katika kipindi cha miaka mitatu ambapo Lesotho imefanya uchaguzi wa mapema.
Ufalme huo pia umeshuhudia majaribio kadhaa ya mapinduzi tangu kupata uhuru wake kutoka kwa Uingereza.
Wiki jana Waziri Mkuu huyo, anayekumbwa na msukusuko wa kisiasa aliambia BBC kwamba serikali yake ya muungano ilikua thabiti.
Hata hivyo mapema leo utawala wake umepata pigo kubwa baada ya bunge kupiga kura ya kutokua na imano naye.
Wanasiasa wengi wa muungano tawala wamehamia kwenye upande wa upinzani na hivyo kuyumbisha utawala wa Waziri Mkuu Pakalitha Mosisili.
Muungano aliounda ulionekana kuwa hafifu sana.
Mwanasiasa huyo alichukua hatamu za uongozi mwaka wa 2015 baada ya uchaguzi mkuu kushindwa kupata mshindi wa moja kwa moja.
Uchaguzi huo ulinuia kutuliza taharuki za kisiasa baada ya jaribio la mapinduzi la Agosti mwaka 2014.
Sasa uchaguzi wa mapema unatarajiwa kufanyika katika kipindi cha miezi mitatu.
Taifa hilo ambalo halina bandari limezungukwa pande zote na Afrika Kusini na uchumi wake hutegemea zaidi mchango wa mataifa jirani.
No comments:
Post a Comment