Kamishna wa Bima, Mamlaka ya
Usimamizi wa Bima Tanzania Bw. Baghayo Abdallah Saqware akiongea na
waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa sekta ya Bima nchini na mikakati
ya kuendeleza na kupanua shughuli za bima nchini, leo Jijini Dar es
salaam. Kushoto ni Meneja Mawasiliano wa mamlaka hiyo Bw. Eliezer
Rweikiza
Meneja TEHAMA, Mamlaka ya
Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Bw. Aron Mlaka akiwaeleza waandishi wa
habari mikakati ya mamlaka hiyo ya kuongeza na kupanua matumizi ya
Teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika kuboresha huduma
zao. Kushoto ni Naibu Kamishna wa Mamlaka hiyo Bw. Juma Makame.
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti
TIRA Bi. Adelaide Muganyizi akifafanua jinsi Mamlaka hiyo inavyotoa
elimu kwa Umma pamoja na umuhimu wa Bima wakati wa mkutano na waandishi
wa habari, leo Jiji Dar es saam. Kushoto ni Naibu Kamishna wa Mamlaka
hiyo Bw. Juma Makame.
(Picha na Georgina Misama).
Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima
Tanzania (TIRA) imejizatiti kurudisha thamani ya huduma za bima kwa
kubadilisha baadhi ya sheria na kanuni za bima pamoja na kutengeneza
mfumo wenye kutoa tija kwa Wananchi, Serikali pamoja na Kampuni za Bima
nchini.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa
Bima, Baghayo Saqware alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya
namna mamlaka hiyo ilivyojipanga kurudisha thamani ya bima kwa wananchi
na makampuni ya bima hapa nchini, leo Jijini Dar es Salaam.
Baghayo Saqware amesema kwamba
moja ya kanuni na sheria zitakazoboreshwa ni pamoja na kupeleka biashara
ya bima (Insurance business – risks) nje ya nchi badala ya kutumia
makampuni ya ndani.
“Tutaweka kanuni itakayolazimisha
Kampuni za bima hapa nchini kuongeza mitaji au kutengeneza mfuko wa
pamoja au mfumo wa makampuni kushirikina kimtaji ili kuweza kuandikisha
na kubakisha sehemu kubwa au biashara yote ya bima nchini,” alifafanua
Saqware.
Aliendelea kwa kusema kuwa
utawekwa utaratibu wa kisheria utakaohakikisha waingizaji wa mizigo
kutoka nje ya nchi wanakatia bima za mizigo yao kupitia kampuni za bima
nchini.
Aidha amesema kwamba ikibidi
mamlaka hiyo itabadilisha sheria ya bima nchini ili wafanyabiashara
wanaoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi (import goods) iwe ni lazima
kukatia bima nchini ili kuongeza mapato ya kodi (VAT) pamoja na bima
(Premium Levy).
Katika kurudisha thamani ya huduma
ya bima kwa wananchi mamlaka hiyo itahakikisha makampuni yanayotoa
huduma ya bima yanatoa huduma stahiki kwa wateja wa bima pamoja na
kuhakikish malalamiko ya wateja yanayofikishwa katika mamlaka husika
yanashughulikiwa kwa wakati.
Aidha, katika kupanua shughuli za
bima mamlaka hiyo iko katika hatua za mwisho za kukamilisha bima ya
kilimo, mifugo pamoja na bima za watu wenye kipato cha chini
(Micro-insurance) pamoja na kukamilisha utekelezaji wa sera ya Taifa ya
Bima.
Vile vile inapanua matumizi ya
teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) kwa kutumia utaratibu wa
kusajili na kutoa leseni za biashara ndani ya siku saba hadi
thelathini, aidha mfumo huo utaondoa tatizo la bima bandia za vyombo vya
moto pamoja na kuhakiki uhalali wa stika za bima kwa walionazo.
Nae, Meneja Tehama TIRA, Aron
Mlaki amesema kwamba mfumo huo wa Tehama utamuwezesha mwananchi kupata
maelezo ya bima yake kupitia intanenti na meseji za kawaida ambapo kwa
upande wa message za kawaida ataandika neno ‘STIKA’ likifuatiwa na
namba ya Stika na kuituma kwenye namba 15200 baada ya hapo atapokea
taarifa za bima yake.
No comments:
Post a Comment