Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limekataa mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Yanga SC na MC Alger ya Algeria kuchezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Aprili 8, mwaka huu kutokana na wenyeji kuchelewesha kuthibitisha mabadiliko ya Uwanja.
Uwanja wa nyumbani wa Yanga unaofahamika na waliouthibitisha ni wa
Taifa, Dar es Salaam, lakini klabu hiyo ilikuwa katika jitihada za
kuuhamishia mchezo huo Mwanza kwa tamaa ya mapato zaidi.
Hata hivyo, tarehe ya mwisho ya kuwasilisha mabadiliko yoyote ya Uwanja
ilikuwa ni juzi wakati Mkaguzi wa CAF, Maxwell Mtonga kutoka Malawi
aliupitisha Uwanja huo jana.
Mtonga alikuwa Mwanza tangu juzi akiongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi katika ukaguzi huo na
ameagiza marekebisho madogo madogo.
Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba, Steven Shijja aliahidi kuhakikisha
wanafanya marekebisho hayo ndani ya muda kama walivyoelekezwa ili mchezo
huo ufanyike Mwanza.
Na tayari mchezo wa Ligi Kuu ya Vodaocm Tanzania Bara kati ya wenyeji
Mbao FC na Simba SC ya Dar es Salaam uliokuwa ufanyike Aprili 8, mwaka
huu Uwanja wa CCM Kirumba, ulikwishasogezwa mbele kwa siku mbili hadi
Aprili, 10.
Yanga SC imeangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa katika
michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Zanaco
Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka nchini Zambia ikitoka kulazimishwa
sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga sasa inaweza kucheza Kirumba iwapo tu itafuzu hatua ya makundi na
pia watatakiwa kuwasilisha mabadiliko ya Uwanja mapema kwa mujibu wa
kanuni.
No comments:
Post a Comment