Na. Georgina Misama MAELEZO
Mtandao wa Vijana
Wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (NYP+) kutoka Bagamoyo Mkoa wa Pwani,
umetoa tamko la kuwataka vijana na wananchi kwa ujumla kuongeza
mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu katika kuadhimisha siku ya
kifua kikuu Duniani.
Akiongea na Waandishi wa
Habari katika kuadhimisha siku hiyo, Mwenyekiti wa NYP+ Bi. Mwanaharusi
Mohamedi anasema kwamba Ugonjwa wa Kifua Kikuu ni hatari lakini
unatibika ikiwa mgonjwa atazingatia tiba na masharti yake.
“Sisi Vijana tunaoishi
na VVU tunawaomba watanzania wenzetu pamoja na wadau wote ambao wapo
katika mapambano dhidi ya kifua kikuu, kufanya kila linalowezekana
kuhakikisha tunautokomeza ugonjwa huu wa Kifua Kikuu” anasema
Mwanaharusi.
Bi. Mwanaharusi
aliongeza kuwa mtu anayeishi na VVU ni rahisi sana kupata maambukizi ya
Kifua Kikuu kwasababu VVU vinapunguza kinga za mwili ambazo zingepambana
na vijidudu vya maambukizi ya Kifua Kikuu.
Aidha, Vijana wa NYP+
wameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kuweka mazingira mazuri na wezeshi
katika kutekeleza mapambano hayo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa
sahihi na ongezeko la vituo vya kutolea dawa hizo.
Akiongolea mikakati ya
serikali katika kupambana na Kifua kikuu Bi. Zulfa Hamisi ambaye ni
mjumbe wa NYP+ anawasihii wananchi wajitokeze kwa wingi kupima na
kupatiwa tiba sahihi ya Kifua Kikuu kwani huduma hizo hutolewa sehemu
nyingi na bila malipo ili taifa letu liweze kutokomeza kabisa Kifua
Kikuu.
“Sisi vijana wa NYP+
tupo tayari kufanya uraghabishi na uhamasishaji pia kutoa elimu juu ya
kupima na kupata tiba ya Kifua Kikuu katika vituo ambavyo serikali
imeviweka kulingana na sera ya afya kitaifa”, anasema Bi. Zulfa.
Dunia huadhimisha Siku
ya Kifua Kikuu Machi 24, kila mwaka, ambapo kauli mbiu ya mwaka 2017
ni “Tuungane pamoja katika kutokomeza kifua kikuu”
No comments:
Post a Comment