Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Maofisa wakuu wa Polisi wanatarajia
kukutana mkoani Dodoma kuanzia jumatatu tarehe 27-29/03/2017 katika
kikao kazi cha siku tatu kujadili na kupanga mikakati mbalimbali ya
kukabiliana na uhalifu na wahalifu hapa nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna
msaidizi wa Polisi ACP Advera Bulimba alisema kikao hicho
kitawakutanisha maofisa wakuu wa makao mkauu ya Polisi, makamanda wa
Polisi wa mikoa na Makamanda wa vikosi bara na Zanzibar ili kujadili
mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utendaji katika kipindi
cha mwaka uliopita na kuweka mikakati mipya ya kupambana na uhalifu kwa
mwaka 2017.
Aidha,
Bulimba alisema mbali na utaratibu wa mawasiliano ya kila siku katika
kuimarisha usalama wa raia na mali zao, Jeshi la Polisi pia lina
utaratibu wa kukutana kila mwaka kwa pamoja ili kubadilishana uzoefu
kukabiliana na wahalifu kwa lengo la kuhakikisha kuwa usalama wa raia na
mali zao unaendelea kuimarika hapa nchini.
“Katika
kikao hicho Inspekta Jenerali wa Polisi IGP Ernest Mangu atatoa
maelekezo ya kiutendaji ambayo lengo lake ni kuhakikisha kuwa kila
ofisa, mkaguzi na askari anawajibika kwa nafasi yake katika kuhakikisha uhalifu unapungua hapa nchini” Alisema Bulimba.
Bulimba
alisema kikao kazi hicho kinatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mhe.Mwigulu Nchemba ambapo kauli mbiu katika kikao hicho
ni “Zingatia maadili tunapopambana na uhalifu ili kuimarisha usalama
kwa maendeleo ya Taifa”.
No comments:
Post a Comment