Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Maafisa Habari na Mawasiliano
Serikalini wametakiwa kutoa taarifa kwa haraka zaidi kwa kutumia njia za
kisasa za mawasiliano ikiwemo tovuti na mitandao ya kijamii ili
kusaidia kutangaza Mafanikio ya Serikali katika maeneo yao ya kazi.
Hayo yamesemwa jana Mkoani Dodoma
na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali
Dkt. Hassan Abbasi, alipokuwa akizungumza na maafisa habari na TEHAMA
katika mafunzo elekezi ya uwekaji wa taarifa katika tovuti
yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na kusimamiwa
na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao (EGA).
Dkt. Abbas alisema kuwa mara baada
ya tovuti kuzinduliwa rasmi, Maafisa Habari wana wajibu wa kuweka
taarifa mpya zinazozingatia muda na wakati kwa kuwa malengo ya tovuti
hizo ni kumsaidia mwananchi kuweza kupata taarifa mbalimbali za
Serikali.
“Tukifungua tovuti hizi tunapaswa
kuona taarifa mpya, kwa sasa suala la upashanaji wa habari na taarifa za
miradi ya Serikali isisubiri tena michakato, isipokuwa kama kutatokea
suala kubwa ambalo litahitaji ufafanuzi kutoka katika ngazi za juu
katika maeneo yenu ya kazi” alisema Dkt. Abbasi
Aliongeza kuwa, taaluma ya habari
katika zama za sasa inahitaji ubunifu mkubwa katika kuisemea Serikali
kwa kutafuta njia mbalimbali za kubaharisha umma badala ya kutumia njia
za kawaida na za kila siku.
“Katika maeneo yetu ya kazi tuna
vituo vya redio na televisheni ambazo zinawahitaji Viongozi wetu kufanya
nao mahojiano maalum kuhusu masuala mbalimbali ya Serikali, ni wajibu
wetu kutumia fursa hizo kuhakikisha tunaisemea Serikali” alisema Dkt.
Abbasi.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi alisema
Serikali itaweka utaratibu maalum wa kupima utendaji kazi wa kila Afisa
Habari katika Wizara, Idara, Taasisi, Wakala na Mamlaka za Mikoa na
Wilaya na Mikoa ili kuona ni namna gani ameweza kutoa taarifa za
Serikali kuhusu masuala mbalimbali ya Serikali.
“Katika kipindi hiki Serikali ya
Awamu ya tano imetekeleza na inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo
ikiwemo miradi ya umeme vijijini (REA), na ujenzi wa miundombinu mingine
kwa kutumia fedha nyingi katika kutekeleza miradi hiyo, hivyo ni wajibu
wa Maafisa Habari kueleza wananchi utekelezaji wa miradi hiyo” alisema
Dkt. Abbasi.
Alisema kuwa ili taarifa hizo za
utekelezaji wa mafanikio hayo ya Serikali ziweze kuwafikia wananchi, ni
wajibu wa Maafisa Habari na Mawasiliano kujenga na kuimarisha mtandao wa
mawasiliano baina yao pamoja na watendaji wengine katika maeneo yao ya
kazi.
Aliongeza kuwa ubunifu ni siri
nyingine ya mafanikio katika suala la upashanaji wa taarifa za Serikali,
hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuwa mbunifu badala ya kulalamika
kutokana na changamoto mbalimbali zinazomkabili katika maeneo yao ya
kazi ikiwemo ufinyu wa bajeti na changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi.
Mafunzo hayo ya wiki moja
yalishirikisha mikoa na Halmashauri za Mikoa ya Arusha, Manyara,
Singida, Dar es salaam, Pwani na Dodoma.
No comments:
Post a Comment