Nimetoka Kituo Kikuu cha Polisi Dar sasa hivi. Polisi wamekataa
kunirudishia simu yangu waliyoinyang'anya kwa nguvu tarehe 6 Machi, siku
waliyonikamata nikiwa mahakamani Kisutu.
Mimi sijatuhumiwa wala kushtakiwa kwa kosa lolote la mtandao chini ya
Sheria ya Makosa ya Mtandao au Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na
Kiposta.
Badala yake nimeshtakiwa kwa makosa ya uchochezi yanayohusiana na kauli
zangu juu ya Serikali ya Rais Magufuli. Aidha, nimeshtakiwa kutokana na
msimamo wangu na kauli zangu juu ya siasa za Zanzibar na masuala ya
Muungano.
Kwa sababu hizi, Jeshi la Polisi halikuwa na, na halina, sababu wala
haki ya kuchukua simu yangu na kuendelea kukaa nayo hadi sasa, siku 17
baadae.
Nimepata taarifa kwamba tangu walipoichukua kwa nguvu karibu wiki tatu
zilizopita, simu hiyo imekuwa inaonekana inatumika kwa mawasiliano ya
whatsapp.
Maana yake ni kwamba polisi wanasoma na au kusikiliza mawasiliano yangu
ya simu na ya kielektroniki. Hii ni kinyume cha sheria za nchi yetu.
Simu hiyo ni chombo changu cha mawasiliano ya kikazi na binafsi. Kama
mbunge, ninaitumia simu hiyo kwa ajili ya mawasiliano yangu na wananchi
walionichagua na viongozi wengine wa kiserikali na kichama.
Jeshi la Polisi halina haki ya kujua au kuingilia mawasiliano hayo.
Kama wakili ninatumia simu hiyo kwa ajili ya mawasiliano na wateja
wangu, wengi wao wakiwa na kesi mahakamani dhidi ya Jeshi la Polisi au
Serikali hii.
Mawasiliano hayo yanalindwa kwa mujibu wa sheria na polisi hawana sababu
wala haki ya kujua au kuingilia mawasiliano hayo na wateja wangu.
Vile vile ninatumia simu yangu kwa mawasiliano yangu binafsi na familia yangu, marafiki zangu na jamaa zangu wengine.
Mawasiliano haya nayo yanalindwa na Katiba yetu na polisi hawana sababu
wala haki ya kujua au kuingilia mawasiliano hayo binafsi.
Kwa vyovyote vile, kitendo cha Jeshi la Polisi kuchukua na kuendelea
kuishikilia simu yangu bila sababu wala haki ni mfano mwingine wa
matumizi mabaya ya mamlaka ya kiupelelezi ya Jeshi hili la Polisi.
Badala ya kushughulikia wahalifu wa wazi kama akina Daudi Bashite na
wenzake, polisi wetu wanahangaika na viongozi waliochaguliwa na wananchi
wanaotumia haki na wajibu wao kikatiba kuikosoa serikali ya Rais
Magufuli kwa sababu ya matendo yake ya hovyo.
Ninafahamu polisi wanafikiri kwamba kwa kunifanyia vitendo hivi basi
nitaogopa na kulegeza msimamo wangu katika masuala mbali mbali
yanayolisibu taifa letu.
Ninawaomba wajiulize kwa nini imeshindikana hadi sasa kulegeza msimamo
wangu huo kwenye masuala hayo, licha ya kunikamata na kuninyanyasa mara
nyingi kwenye vituo vya polisi na mahakamani. Sitishiki na sitatishika
na mambo yao haya.
Hata hivyo, naomba niseme wazi ili mwenye kusikia na asikie. Vitendo
hivi vya Jeshi la Polisi havifai na vinatakiwa kukoma kabisa. Polisi
wanirudishie simu yangu mara moja na bila masharti yoyote.
Ninaendelea kutafuta mawasiliano ya IGP Mangu na wakubwa wenzake ili wanieleze kwa nini simu yangu inashikiliwa na maofisa wao.
Endapo na wao watashindwa kutoa maelekezo sahihi kwa waliochukua simu
yangu na wanaendelea kukaa nayo, nitalazimika kwenda Mahakama Kuu ili
kuomba mahakama iingilie kati na kutamka kama ni sahihi kisheria kwa
mapolisi wa nchi hii kuingilia mawasiliano ya sisi wananchi kwa namna ya
hovyo namna hii.
Naomba mnaopata ujumbe huu mnisaidie kupaza sauti zetu ili matendo haya mabaya yakome katika nchi yetu.
Wasalaam,
Mh. Tundu AM Lissu
No comments:
Post a Comment