Na. Georgina Misama – MAELEZO
Serikali imewataka
wamiliki wa ardhi kuhakikisha wanalipia kodi ya pango la ardhi kwa
wakati ili kuepuka kunyang’anywa umiliki wa ardhi zao.
Hayo yamesemwa na Mkuu
wa Kitengo cha Mawasilino kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Bi. Mboza Lwandiko wakati akizungumza na waandishi wa habari,
Jijini Dar es Salaa.
Mboza alisema kwamba
Wizara inakusudia kufanya mnada wa viwanja takribani 10 kutoka
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Temeke na Kinondoni ambavyo
havijalipiwa kodi ya pango la ardhi mpaka Machi 24, 2017.
“Usipolipa Kodi ya Pango
la Ardhi kwa wakati, utanyanganywa umiliki wa ardhi yako, kutokana na
sheria ya Ardhi, Na. 4 ya mwaka 1999, katika kifungu cha 49 na 51”,
alisema Mboza.
Naye Mkuu wa Kitengo cha
Kodi kutoka Wizara hiyo Bw. Denis Masami alitoa ufafanuzi wa utaratibu
unaotumika kuwasiliana na wamiliki wa ardhi walioshindwa kulipa kodi
kwa wakati na kusema kwamba wadaiwa wanapewa hati ya madai na kupewa
muda wa kukamilisha madeni yao.
Muda wa kukamilisha
malipo ukipita, amri ya mahakama ya kukamata mali hufuata, ambapo
mmiliki wa ardhi atatakiwa kuikomboa ardhi yake kwa kulipa deni mara
moja, akishindwa Mahakama hutoa amri ya kuuza mali.
Mahakama imetoa amri ya
kwanza tarehe 27/01/2017 ya kukamata mali kwa wadaiwa sugu na tarehe
24/01/2017 mahakama ilitoa kibali kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kuuza kwa mnada wa hadhara viwanja ambavyo
havijalipiwa kodi ya pango la ardhi.
“Tarehe 20 Machi, 2017
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilitoa tangazo la mnada wa
hadhara wa kuuza viwanja ambavyo havijalipiwa kodi ya ardhi
unaotarajiwa kufanyika Machi 26, 2017”, alisema Denis.
Denis aliongeza kwamba
Wizara imeandaa orodha ya wadaiwa sugu, mpaka sasa katika orodha hiyo
baadhi ya viwanja vimelipiwa sehemu ya kodi inayodaiwa baada ya wamiliki
kuomba kukamilisha sehemu iliyobaki kabla ya kumalizika kwa muhula huo.
Wizara inatoa rai kwa
watanzania wanaomiliki ardhi kujifunza utamaduni wa kulipia kodi pasipo
shurti. Kodi ya ardhi hulipiwa kila ifikapo Julai Mosi ya kila mwaka
katika Manispaa au Halmashauri husika na katika Ofisi za Malipo ya
Kodi-Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment