Na: LilianLundo – MAELEZO
Serikali imefuta usajili wa vibali
vya uzalishaji na Uingizaji wa aina 20 ya pombe kali za viroba
zilizokuwa zimesajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii
Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo, Jijini Dar es
Salaam kuhusu usitishaji wa uzalishaji na uingizaji, uuzaji na matumizi
ya pombe zilizofungwa katika mifuko ya plastiki (Viroba).
“Tumefuta usajili wa vibali vya
uzalishaji na uingizaji kutoka nje, usambazaji, uuzaji na matumizi ya
pombe kali zilizofungashwa katika mifuko ya plastiki (viroba) chini ya
ujazo wa milimita 200,” alifafanua Ummy Mwalimu.
Aliendelea kwa kusema kuwa hatua
hiyo ni utekelezaji wa tamko la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilotoa
Februari 02, 2017 la kusitisha uzalishaji, uingizaji, usambazaji, uuzaji
na matumizi ya pombe hiyo kali kuanzia Machi 01, 2017.
Ummy amesema kuwa usitishaji huo
unazingatia kanuni za kukataza uzalishaji, uingizaji na matumizi ya
vifungashio vya plastiki kufungashia pombe kali za mwaka 2017 (The
Environmental Management (Prohibition of Manufacturing, Important and
Use of Plastic Sachets for Packakging Distilled and other alcoholic
beverages) Regulations 2017) imekatazwa kutumia vifungashio vya plastiki
kufungashia pombe kali. Badala yake wazalishaji watapaswa kufungasha
pombe kali hizo katika chupa zenye ujazo usiopungua mililita 200.
Aidha amesema kuwa uamuzi wa
kupiga marufuku matumizi ya pombe za aina hiyo unatokana na athari
mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kiafya na kijamii.
Matumizi mabaya ya pombe hizo
yamesababisha ajali nyingi, vifo, ulemavu na mzigo mkubwa kwa Serikali
wa kutoa huduma kwa wahanga wa pombe hizo na ongezeko la makosa ya
jinai.
Ummy amesema kwamba Viroba vilivyokamatwa na kuzuiwa vinasubiri maelekezo kutoka ofisi ya Waziri Mkuu namna ya kuviteketeza.
No comments:
Post a Comment