Thursday, 2 March 2017

Namna ya kupunguza vifo kwa akina mama kutokana na matatizo ya mimba, uchungu na uzazi

    9-washiriki wa mamamnadamano wakisikilia hotuba ya Mmama Salma Kikwete
Na Jovina Bujulu- MAELEZO.
Utepe mweupe duniani ni alama ya uwakilishi ya kuwakumbuka akina mama waliofariki kutokana na matatizo ya mimba, uchungu na uzazi pamoja na utepe mweupe ili kushughulikia matatizo yanaweza kuepukika kwa akina mama.
Nchini Tanzania asasi ya kiraia ya Muungano wa Utepe mweupe ndiyo inashugulikia huduma mbalimbali za afya na kuhamasisha jamii kuwajibika ili kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi.
Mratibu wa taifa asasi hii Mama Rose Mlay akizungumza jijini Dar-es-Salaam hivi karibuni alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa asasi hii ni kushawishi kuimarika kwa huduma za afya, kwa mama na mtoto.
“Asasi hii ambayo ilianzishwa mwaka 2004 pia inahakikisha kuwa tatizo la vifo vya uzazi linapunguzwa na hatimaye kumalizwa kabisa, hasa kutokana na sababu ambazo zinaepukika” alisema mama Mlay.
Aliendelea kusema kuwa lengo la asasi hii pia kuifanya Tanzania kuwa taifa ambalo haki ya mama na mtoto kuwa salama wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua linazingatiwa.
Inakisiwa kuwa duniani kiasi cha wanawake 8000 hufanikiwa kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi. Idadi hii ya watu ni kubwa kwa viwango vyovyote vile na ina madhara makubwa kijamii na kiuchumi.
Utafiti wa demokrasia ya Afya wa mwaka 2010, ulionyesha kuwa wanawake 24 hufariki kila siku na watoto wachanga 144 hufariki kila siku. Kutokana na juhudi za serikali, Muungano wa Utepe mweupe na wadau wake, vifo hivyo vilipungua kwa wajawazito 600 na watoto chini ya mwezi mmoja vifo 1000 vilipungua ikilinganishwa na mwaka 2013 ambapo wajawazito waliopoteza maisha walikuwa 8500 na watoto 48000 kwa mwaka.
“Vifo hivyo vina madhara makubwa kwa kijamii na kiuchumi kwani wanaokufa ni nguvu kazi ya taifa, na vifo hivyo huacha watoto yatima ambao wanaleta changamoto kubwa kwa jamii katika malezi” anasema Mama Mlay.
Sababu za vifo hivyo ni pamoja na uduni wa huduma za afya, utaratibu wa kujifungulia nyumbani, gharama zinazoambatana na huduma hizo, kifafa cha mimba na mapigo ya moyo kuwa juu.
Katika maadhimisho ya siku ya Utepe mweupe yaliyofanyika mwaka 2016, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan aliwasihi wanawake kujiunga na mfuko wa jamii wa huduma ya Bima ya Afya ili kuondokana na ukosefu wa fedha wakati wa kujifungua maana huduma hii inatolewa kwa utaratibu maalum unaowawezesha kutibiwa bila kulipa fedha taslimu.
Aidha Mama Samia aliwataka wananchi kuachana na mila potofu hasa ukeketaji ambao unasababisha tatizo la kutoka damu nyingi na hatimaye kusababisha vifo wakati wa kujifungua.
Vikwazo vingine vya kufikiwa uzazi salama nchini ni pamoja na vituo vingi vya afya kukosa huduma za awali na za dharura, kama upasuaji na damu salama, umeme wa uhakika, hasa vijijini na upungufu wa watumishi wa afya wenye ujuzi na stadi, upungufu wa vifaa, tiba na dawa muhimu.
Changamoto nyingine ni pamoja na kuwanyima watoto wa kike elimu, kuwaozesha watoto katika umri mdogo, kuwanyima wanawake fursa ya kumiliki uchumi, hivyo kuwafanya kushindwa kufikia huduma bora za afya hususani wakati wa kujifungua na kuishia kuhudumiwa na wakunga wa jadi ambao hawawezi kuhimili matatizo makubwa ya uzazi pindi yanapojitokeza.
Naye Afisa mawasiliano wa asasi hiyo Ndugu Anna Sawaki anasema kuwa asasi hiyo inafanya kazi kwa karibu sana na kundi la wabunge 22 wakiongozwa na Mbunge wa Peramiho Mh Janista Mhagama, kwa kushawishi watunga sera waongeze bajeti ya wizara ya Afya ili kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na kutoa elimu ya uzazi ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
“Katika kuhakikisha tunafanikisha suala hilo, Muungano wa Utepe mweupe umekuwa ukitafuta ushawishi ngazi ya halmashauri mpaka serikali kuu kwa nafasi zao kuhakikisha bajeti ya huduma za uzazi za dharura zinapewa kipaumbele katika ngazi za halmashauri na bajeti ya afya kwa ujumla” anasema Ndugu Sawaki.
 
Mikakati inayofanywa na Muungano wa Utepe mweupe ni pamoja na kushirikiana na mashirika mbalimbali katika kuhakikisha kampeni hii inawafikia walengwa. Mfano ni asasi ya AFRICARE ambayo itajenga chumba cha upasuaji mkoani Rukwa na asasi ya Benjamini Mkapa ambayo imeendelea kutoa mafunzo ya huduma za afya na asasi nyingine ambazo zinasaidia kuimarisha miundombinu kama umeme na maji.
Aidha Muungano huu pia wamefanya kampeni mbalimbali za kuongeza watumishi wa afya katika vituo vya kutoa huduma, kuboresha huduma katika mikoa ya pembezoni na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi. Kampeni hii imefanikiwa katika mkoa wa Rukwa, ambapo idadi ya wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya afya imeongezeka kwa asilimia 65 mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 30 mwaka 2010.
Baadhi ya wananchi wameipongeza asasi hii na kushauri elimu ya uzazi itolewe kwa msukumo zaidi hasa kwa wanawake wa vijijini. Pia wizara ya afya imeshauriwa kufuatilia kwa karibu hospitali za binafsi ambazo nyingine huajiri watumishi wasio na utaalamu wa kutosha jambo ambalo ni kikwazo kwa wajawazito kipindi cha kujifungua.
Mama Mlay alitoa wito kwa jamii kuleta mabadiliko katika kumkomboa mwanamke na changamoto anazokabiliana nazo ili kuongeza kasi ya kupunguza vifo vya uzazi na wakati huohuo kuokoa maisha ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Hii itasaidia kujenga jamii yenye siha zaidi itakayounganisha nguvu zake katika kuleta maendeleo ya Taifa kwa umoja wake.
Baadhi ya Mashirika, taasisi na asasi zinazoshirikiana na Muungano wa Utepe mweupe ni pamoja na AFRICARE, TAMA, UMATI, Plan International, Thamini Uhai, Mkapa Foundation na Save the Children.
Asasi hii inashirikiana na nchi wanachama kutoka Uingereza, India, Malawi, Nepal, Nigeria, Sweden, Uganda, Yemen, Zimbabwe, India na Afghanistan.
Kila tarehe 15 Machi Muungano wa Utepe Mweupe hufanya maadhimisho ya siku ya Utepe mweupe ambapo hufanya shughuli mbalimbali, kama vile kutoa ushauri wa afya ya uzazi, na upimaji wa magonjwa mbalimbali.
Mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika tarehe 10 Machi ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan lakini yatatanguliwa na shughuli ya kupanda mlima Kilimanjaro itakayoanza tarehe 5, Machi mpaka tarehe 9, Machi. Watakaohusika na kupanda mlima huo wataomba ufadhili na pesa zitakazopatikana zitalenga kujenga chumba kimoja cha upasuaji . Kauli mbiu ya mwaka huu itakuwa ni “VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI HAVIKUBALIKI WAJIBIKA.”

No comments:

Post a Comment