Friday 24 March 2017

Mbwana Samatta:Tunataka kuutumia mchezo wa Jumamosi (kesho) kuongeza ubora kwenye viwango vya FIFA

Nahodha wa timu ya Taifa 'Taifa Stars', Mbwana Samatta, amesema umoja wa wachezaji wenzake na mashabiki unaweza ukawapa ushindi kwenye mchezo wa kesho wa kirafiki dhidi ya Botswana.
Samatta, alisema kuwa mchezo huo si mwepesi kama watu wanavyouchukulia kwa kuwa wapinzani wao nao wanauwezo wa kutosha.
"Mimi nafikiri tunapaswa kuungana kwa ajili ya mchezo huu, tunaendelea na maandalizi na makocha wamekuwa makini muda wote kwenye mazoezi, mashabiki na Watanzania wote tuungane kuelekea kwenye mchezo huu," alisema Samatta.
Alisema ushindi kwenye mchezo huo utawasaidia kupanda kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
"Tunataka kuutumia mchezo wa Jumamosi (kesho) kuongeza ubora kwenye viwango vya FIFA ndio maana tunajiandaa na tunajipanga kushinda," aliongezea kusema Samatta anayecheza soka la kulipwa kwenye klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.



Baada ya mchezo wa kesho, Stars itacheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Burundi Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Michezo hiyo yote ya kirafiki ipo kwenye kalenda maalum ya FIFA.

No comments:

Post a Comment