Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim
Yong Kim, atafanya ziara ya kikazi nchini kuanzia tarehe 19 hadi 21
Machi 2017. Akiwa nchini, Dkt. Kim atafanya mazungumzo na Mhe. John
Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu
Jijini Dar Es Salaam siku ya Jumatatu, tarehe 20 Machi 2017 pamoja na
kushiriki uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Barabara za Juu katika
eneo la Ubungo (Ubungo Interchange).
Katika mazungumzo yao,
Viongozi hao watajadili namna bora ya kuimarisha zaidi uhusiano uliopo
kati ya Tanzania na benki hiyo. Vilevile, watazungumzia miradi mikubwa
inayotarajiwa kutekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia katika kipindi
kijacho.
Aidha, baada ya mazungumzo
hayo, Rais Magufuli na mgeni wake watashuhudia uwekwaji saini wa
mikataba mitatu: (i) Uboreshaji Miundombinu ya Usafiri Jijini Dar es
Salaam ikiwemo awamu ya tatu na ya nne ya mradi wa DART pamoja na ujenzi
wa barabara ya juu katika eneo la Ubungo (Dar es Salaam Urban Transport
Project (DUTP); (ii) Awamu ya pili ya mradi wa Uboreshaji wa
Upatikanaji wa Maji safi na uboreshaji wa miundombinu ya maji taka
(Water and Sanitation Project) na (iii) Uboreshaji wa Miundombinu na
Huduma za msingi katika baadhi ya miji (Tanzania Strategic Cities
Project).
Wakati wa ziara hiyo, Dkt. Kim
atapata pia fursa ya kutembelea Shule ya Msingi Zanaki ambayo ni moja
ya Shule zinazonufaika na mpango wa kuboresha ubora wa elimu ya msingi
unaogharamiwa na Benki ya Dunia.
Ziara ya Dkt. Kim inafuatia
ziara iliyofanywa nchini na Makamu wa Rais wa Benki hiyo wa Kanda ya
Afrika, Bw. Makhtar Diop mwezi Januari 2017 ambapo alishiriki uzinduzi
wa mradi wa mabasi ya mwendo kasi (BRT) uliofanyika kwenye kituo kikuu
cha mabasi hayo kilichopo Kariakoo jijini Dar Es Salaam.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 17 Machi, 2017
No comments:
Post a Comment