Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Pombe kali zilizofungashwa katika
vifungashio vya plastiki maarufu kama ‘viroba’ zenye thamani ya
shilingi Bilioni 10.8 zimekamatwa Jijini Dar es Salaam katika msako wa
pombe hizo uliofanyika kuanzia Machi 01 mpaka 03, mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba leo
Jijini, Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu
operesheni ya utekelezaji wa maelezo ya Serikali ya kusitisha pombe hizo
za viroba hapa nchini kuanzia Machi 01, mwaka huu.
“Jumla ya katoni 99,171 za pombe
kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (Viroba)
zimekamatwa ambapo katoni 69,045 ni zenye ujazo wa na mililita 50,
katoni 29,344 zenye ujazo wa mililita 100, katoni 782 zenye ujazo wa
mililita 90 pamoja na katoni 10,625 za chupa zenye ujazo wa mililita
100. Thamani yake ni Shilingi Bilioni 10.83,” alifafanua Makamba.
Aliendelea kwa kusema kuwa, jumla
ya viwanda 16 vya kuzalisha pombe kali, maduka ya jumla 18, maghala 4,
baa 3 na kiwanda kimoja cha kuzalisha bidhaa za plastiki ikiwemo
vifungashio vya plastiki vya kufungashia viroba vilikaguliwa katika
opesheni hiyo.
Makamba amesema kuwa, pombe
zilizokamatwa zimezuiliwa kuuzwa au kusambazwa kutoka katika maeneo
ambayo yamehifadhiwa yaani viwanda, maghala pamoja na maduka ya jumla
mpaka hapo Serikali itakapotoa tamko.
Aidha wananchi wametakiwa
kushiriki katika utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa kutoa taarifa
zitakazowezesha kubaini wanaokaidi agizo la Serikali la kuzalisha,
kusambaza, kuuza au kutumia pombe hizo kupitia namba ya simu 0685 333 444 kwa kutuma ujumbe mfupi wa meseji au whatsapp au kwa kupiga simu.
Vile vile amesema kuwa zawadi
kati ya shilingi laki 5 hadi milioni 1 zitatolewa kwa mwananchi
atakayetoa taarifa itakayowezesha kukamatwa na kushtakiwa kwa mtu yeyote
mwenye ghala au aliyehifadhi shehena ya pombe za viroba kinyume cha
sheria, watu au mtu anayeingiza pombe za viroba nchini kutoka nje ya
nchi kinyume na sheria na utaratibu, anayehamisha au kusafirisha pombe
za viroba kinyume na sheria, mtu mwenye kiwanda/mtambo wa kuzalisha
pombe za viroba ambao hautambuliki na Serikali pamoja na mtu anayetumia
stempu feki za TRA .
Pombe za viroba zimechangia kwa
kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira, kupotea kwa nguvu kazi ya Taifa,
ajali na vifo vinavyosabaishwa na unywaji uliokithiri wa pombe hizo,
kuongezeka kwa vitendo vyauhalifu na kupotea kwa mapato yanayosababishwa
na wafanyabiashara wasio waamini.
Kutokana na athari hizo, Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alipokuwa Mkoani
Manyara, Februari 16 mwaka huu alitoa tamko la kusitisha uzalishaji,
usambazaji, uuzaji na utumiaji wa pombe kali za viroba kwa nchi nzima
kuanzia Marchi 01, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment