Mwanasheria mkuu wa Marekani, Jeff Sessions, alikutana kwa zaidi ya mara
mbili na balozi wa Urusi wakati wa kampeni za urais za Donald Trump
mwaka uliopita, Serikali imethibitisha.
Sessions ambaye wakati huo alikuwa ni seneta, hakuweka wazi mkutano wake
na balozi wa Urusi wakati alipohojiwa na wabunge wakati wa
kuthibitishwa kwake kama mwanasheria mkuu.
Hata hivyo amesisitiza kuwa hakuwahi kukutana na kiongozi yeyote wa Urusi kuzungumzia masuala ya kampeni.
Kiongozi wa wachache bungeni kutoka chama cha Democrats, Nancy Pelos,
amemtumu Sessions kwa kudanganya wakati akiwa chini ya kiapo na kumtaka
ajiuzulu nafasi yake.
Wabunge wengine wamemtaka aachie nafasi yake kupisha uchunguzi wa
shirika la upelelezi FBI, ambalo linamchunguza mwanasheria mkuu kuhusu
madai haya mapya dhidi yake.
Taarifa hizi zimeibuka punde tu baada ya bunge la Congress kukubali
kufanyike uchunguzi rasmi kuhusu madai kuwa Urusi iliingia uchaguzi wa
nchi hiyo kwa kufanya udukuzi.
Kamati ya masuala ya intelijensia inatarajia kuwachunguza na kuwahoji
maofisa wa Serikali ya Trump pamoja na watu wake wa kampeni kuhusiana na
kufanya mawasiliano na Urusi.
Ikulu ya Marekani yenyewe imekanusha kuwepo kwa mgongano wowote wa
kimaslahi wala jambo baya lililofanywa wakati wa kampeni za urais mwaka
uliopita.
Hata hivyo nchi ya Urusi imeendelea kukanusha shutuma zinazoelekezwa dhidi yake.
No comments:
Post a Comment