Wednesday, 1 March 2017

Mamalaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imewashauri wananchi na Mamlaka za Miji kuhakikisha kuwa mifumo na njia za kupitisha maji

 index
Na : Mwandishi Wetu
Mamalaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imewashauri wananchi na Mamlaka za  Miji kuhakikisha kuwa mifumo na njia za kupitisha maji katika maeneo yao inafanyakazi kwa kiwango cha kutosha ili kuepuka madhara yanayowezo kutokana na mvua za msimu zinazotarajiwa kuanza Mwezi Machi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamalaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) Dkt. Agnes Kijazi ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa msimu wa mvua Tanzania katika kipindi cha mvua za masika kuanzia Machi hadi Mei.
Amesema kuwa yapo maeneo ambayo yatapata mvua za wastani na juu ya wastani na wengine chini ya wastani ni vema wananchi wakachukua tahadhari ili kuepuka madhara mbalimbali ambayo yanaweza kuwapata kutokana na mvua hizo.
Dkt. Kijazi ameongeza kuwa mvua hizo zinaweza kusababisha maji kutuwama katika baadhi ya maeneo ya hivyo kusababisha mafuriko ambayo yatapelekea kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko na uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo mifumo ya maji na barabara.
Aidha ,Mkurugenzi Mkuu amesema kuwa hali ya unyevunyevu katika udongo inatarajiwa kuimarika kiasi cha uzalishaji wa malisho ya mifugo  na ukuaji wa mazao katika baadhi ya maeneo kuongezeka .
Hata hivyo , Mkurugenzi Mkuu huyo amewashauri wafugaji kuwa na mifugo ambayo inalingana na uwezo wa malisho yaliyopo kulingana na ushauri wa Maafisa Mifugo.
Vile vile ameshauri wananchi kuzingatia taratibu za uvunaji , uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali ya maji katika maeneo ambayo yatapata mvua za wastani na chini ya wastani ili kuwa na hifadhi ya kutosha ya maji kwa ajili ya matumizi ya baadaye wakati wa shida ya maji.
Dkt. Kijazi alimeyataja maeneo ambayo yanatarajiwa kuwa mvua ya wastani na juu ya wastani kuwa ni Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya na Iringa.
Maeneo ambayo yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani ni njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, na kusini mwa Morogoro.
Amesema kuwa ukanda wa Ziwa Victoria na maeneo ya pwani ya Kaskazini mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuungana na msimu wa Machi na kusambaa katika maeneo mengine.
 
Dkt. Kijazi amesema kuwa maeneo ya  Arusha, Manyara na Kilimanjaro , Tanga, Dar es Salaam, Kaskazini mwa Morogoro na Visiwa vya Unguja na Pemba yanatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani na vipindi virefu vya ukavu.

No comments:

Post a Comment