Makamu wa Rais wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, aliyeambatana na Azam FC kuelekea
mchezo wake wa marudiano dhidi ya Mbabane Swallows, amesema wanauhakika
mkubwa wa timu hiyo kusonga mbele kwa raundi ijayo ya Kombe la
Shirikisho Afrika.
Karia ameambatana na kigogo
mwingine wa TFF ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho
hilo, James Muhagama, wote kwa pamoja wakiwa na imani kubwa na timu hiyo
ambayo iliondoka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani.
Azam FC inakabiliwa na mchezo huo
muhimu utakaofanyika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo, mjini Mbabane,
Swaziland Jumapili hii saa 10.30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki,
ambapo inahitaji ushindi wowote au sare yoyote ili kuweza kusonga mbele.
Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz,
Karia alisema kuwa mchezo huo ni muhimu kwa Azam FC kuweza kushinda,
huku akidai kuwa ina mahesabu mazuri kutokana na kuondoka na ushindi
katika mchezo wa kwanza.
“Ukiangalia kimahesabu wao ndio
wanamahesabu mazuri, na ndio maana hapa kuna uwakilishi mzito umekuja
kutoka TFF tupo wawili, tunauhakika ya kwamba tutafanya vizuri, Azam FC
kwa sasa wapo vizuri,” alisema.
Karia alitoa ushauri kwa wachezaji
wa timu hiyo kuzingatia nidhamu ya mchezo wakiwa uwanjani huku
akiwataka wahakikishe wanapata bao mapema ili kuuweka mchezo kuwa mgumu
kwa wenyeji.
“Kwa hali hiyo sisi tunauhakika
kabisa Azam FC wapo katika nafasi nzuri ya kupita na mambo mengine
tunamwachia Mungu, cha msingi wachezaji wa Azam FC wawe na nidhamu ya
mchezo ya kujua kuwa wanacheza ugenini na nadhani mwalimu atakuwa
amelichukulia uzito, Azam FC sio wageni kwenye michuano ya kimataifa,
karibu wanamiaka mine sasa wanashiriki na makosa waliyojifunza nyuma
huko watayarekebisha ili waweze kupita,” alimalizia.
Azam FC inaelekea kwenye mchezo
huo ikiwa na morali kubwa jambo ambalo linatoa mwanga kwa timu hiyo
kuweza kusonga mbele kwa hatua ya mwisho ya mtoano, ambayo itakutana na
moja ya timu 16 zilizotolewa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa
Afrika kabla ya kuingia hatua ya makundi.
No comments:
Post a Comment