Serikali imetaka Shule Binafsi Kuwa na Mihula Miwili ya Masomo
WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi imeziagiza shule zote za binafsi kuwa na Mihula miwili tu ya
masomo kwa mwaka badala ya kuwa na mihula mitatu au minne kama ilivyo
kwa sasa katika shule hizo.
Agizo hilo liko kwenye Waraka wa Elimu
Namba Moja wa Mwaka 2015, ambao unaeleza kuwa kuanzia sasa mihula ya
masomo, itakuwa miwili kwa kila mwaka wa masomo kwa shule zote za Serikali na zisizo za Serikali.
Waraka huo uliosainiwa na Kamishna wa
Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa umefafanua kuwa kila muhula, utakuwa
na likizo fupi na likizo ya mwisho wa muhula. Siku za masomo kwa mwaka
zitakuwa ni 194.
Waraka huo pia umeagiza wanafunzi wote,
wapumzike mwezi Juni na Desemba na Mashindano ya michezo ya shule za
msingi (Umitashumta) na michezo ya sekondari (Umiseta), ifanyike mwezi
Juni wakati wa likizo.
Kutokana na agizo hilo, wamiliki wa
shule zisizo za serikali wametakiwa kuwasilisha wizara ya Elimu kalenda
za mihula ya masomo. Nakala ya waraka huo wamesambaziwa wakaguzi wote Wa
shule, walioko kwenye kanda na wilaya kuhakikisha wanazifuatilia shule
zote ili ziweze kutii agizo hilo la Serikali.
Profesa Bhalusesa alifafanua katika
waraka huo, umekazia Waraka wa Serikali Namba 5 wa Mwaka 2012 ambao
ulikuwa unaelekeza mihula ya masomo kwa shule za sekondari na vyuo Vya
ualimu, ifanane ili kuepusha usumbufu kwa walimu na kwa wanafunzi.
No comments:
Post a Comment