Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Wanafunzi wa Chuo cha Ualimu wa Elimu Maalum Patandi, mkoani Arusha jana walifanya vurugu zilizowalazimisha Polisi kuwasambaratisha kwa mabomu.
Wanafunzi waligoma na kufunga barabara kuu ya kutoka Moshi -Arusha
kwa kutumia mawe kwa takribani saa moja kuanzia saa 4 hadi 5 asubuhi.
Wakizungumza na NIPASHE chuoni hapo jana, wanafunzi hao walisema lengo la mgomo wao ni kushinikiza mkuu wa chuo aondolewe.
“Chanzo cha vurugu hizi ni kufikisha kilio chetu kwa ngazi za juu,” alisema mwanafunzi mmoja.
Alidai mkuu wa chuo hicho Zaina Mbelwa, anawapa adhabu za shule za
msingi kama kuwapigisha magoti, kuwapiga makofi na kuwafanyisha usafi
wakati wanatoa Sh. 30,000 za kufanyiwa usafi.
Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Usa River, Msolo Msolo, alisema
walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi na kutuliza
hali ya hewa.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Chuo Mbelwa, alisema wanafunzi hao
walifanya hivyo kwa sababu ya kuwabana ili wafuate sheria na kanuni za
chuo.
Alisema baadhi ya wanafunzi wanavuta bangi na kutumia dawa za kulevya na hivyo kuvunja sheria na kanuni za chuo.
Pia alisema baadhi yao wanajiingiza katika mahusiano ya kimapenzi
na walimu badala ya kufuata masomo na pale wanapolazimika kuwakagua
wanagoma.
Kuhusu fedha za usafi, alisema wanalipa Sh. 15,000 na sio Sh. 30,000 kama wanavyodai.
Alikiri kuwaadhibu wanafunzi wanaokiuka sheria na kanuni tena wengine hawahudhurii masomo na badala yake wanasikiliza redio.
Kuhusu chakula, alisema kuna tatizo ambalo sio lake, ni la mzabuni
ambaye amegoma kuleta mboga akidai hajalipwa Sh. milioni 220 za mwezi
Machi.
Akizungumzia kuhusu uongozi wa wanafunzi, alisema wanafunzi hao hawana uongozi na ndio maana tatizo hilo limejitokeza.
Katika mazungumzo na polisi jana, walimshauri kuitisha uchaguzi wa viongozi wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo mapema.
Alisema baada ya kumaliza mitihani siku tano zijazo, ataitisha uchaguzi.
Baadhi ya walimu walisema kwa nyakati tofauti kuwa mkuu wa chuo ndio tatizo.
Walidai mwa mfano, mkuu wa chuo ndiye afisa masurufu na ndiye
anayesaini akaunti za shule na pia amewatenga walimu na kila kitu
anafanya mwenyewe.
Walidai pia amekuwa akiwagawa kikanda, dini pale safari zenye kulipwa marupurupu zinapopatikana.
Walisema kilio hicho kimefikishwa ngazi nyingi ila hawasilikilizwi na matokeo yake walimu wanahoji wanaitwa Ukawa.
(Ukawa ni Umoja wa Katiba ya Wananchi ambao ulianzishwa na vyama
vya upinzani katika kipindi cha Bunge Maalum la Katiba kupinga mchakato
huo).
No comments:
Post a Comment