Thursday, 23 April 2015

Msafara wa Chenge wadaiwa kufurumusha risasi Chadema.

Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, wanadaiwa waliingia ‘anga’ za ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Bariadi na kusababisha taharuki kubwa, baada ya mmoja wa wafuasi wake kudaiwa kufyatua risasi tatu hewani. Tukio hilo lilitokea katika ofisi za Chadema juzi saa 1:30 jioni baada ya wafuasi wa Chadema kumsindikiza mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec), John Heche, aliyetoka kumsindikiza Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama hicho, John Mnyika, aliyekuwa akienda wilayani Maswa kwa shughuli za kichama.
 
Msafara wa Chenge ulikuwa ukitokea katika mkutano kwenye kijiji cha Isanga, na wale wa Chadema wakiwa wamerudi toka mkutano uliofanyika viwanja vya Basketi mjini hapa, ndipo walipokutana na msafara wa Chenge jirani na ofisi za Chadema na kuanza mabishano. 
 
Inadaiwa msafara wa Chenge ulisimama katika ofisi hizo ukiwa na magari matano, huku moja ya magari hayo likipiga muziki kwa sauti kubwa, hali iliyosababisha wafuasi wa Chadema kuurushia mawe  na kuwazomea.
 
KAULI YA POLISI
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Gemini Mushi, alisema vyama hivyo baada ya kumaliza mikutano yao, Chadema walianza safari ya kuelekea ofisini kwao katika barabara ya Maswa, huku msafara wa Chenge ukitokea kijiji cha Isanga kurejea mjini.
 
Alisema baada ya msafara wa Chenge kufika jirani na ofisi za Chadema walikutana na kundi kubwa likishangilia, ndipo mbunge huyo aliposhuka katika gari na kuanza kucheza nao, lakini wakati wafuasi hao wakiendelea kushangilia, walisikia sauti ikisema rusha mawe iliyosababisha mbunge huyo kukimbilia ndani ya gari.
 
Kamanda Mushi alisema baada ya wafuasi hao wa Chadema kurusha mawe kwa kulishambulia gari la Chenge, ndipo kada wa CCM (jina tunalihifadhi kwa sasa) alipotumia bastola yake kurusha risasi tatu hewani ili kuwatanya watu waliokuwa wamezingira msafara huo na watu hao kutawanyika.
 
Hata hivyo, kamanda huyo hakueleza kama mtu huyo amekamatwa na kama kuna ganda lolote la risasi ambalo polisi waliliokota.
 
MASHUHUDA WANENA
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, walisema wafuasi wa Chadema walianza kurusha mawe ndipo mbunge huyo alipokimbilia ndani ya gari yake.
 
“Tulishangaa kuona wafuasi wa vyama hivyo wakianza kushambuliana kwa mawe baada ya kutokea kwenye mikutano yao ya hadhara na kufika maeneo hayo,” alisema Mkuba Majaliwa.
 
VIONGOZI WA CHADEMA
Akizungumzia tukio hilo, John Heche, alisema wafuasi wa CCM walipita katika ofisi za chama chao na kukutana na viongozi pamoja na wafuasi waliotoka mkutanoni huku CCM wakipiga muziki, hali ambayo ilisababisha baadhi ya viongozi kuwazuia kwa madai ya kuwataka kupunguza sauti ya muziki.
 
“Msafara huo ulifika ofisi ya Chadema baada ya kutoka katika mikutano yao na ulipofika maeneo ya ofisi zetu walisimamisha magari yao na kuanza kupiga muziki na wafuasi wao waliteremka kwenye magari yao na kuanza kucheza hali iliyosababisha wafukuzwe kwa mawe na wafuasi wa chama changu,” alisema Heche.
 
VIONGOZI WA CCM
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Wilayani Bariadi, Sai Samba, alisema baada ya kufika jirani na ofisi ya Chadema walikuta kundi la vijana wakiwa wamejipanga barabarani na kuzuia msafara wao kwa kurusha mawe mbele ya gari la Chenge, hali iliyomlazimu mmoja wa wafuasi wa Chenge kurusha risasi hewani kwa lengo la kuwatawanya.
 
Hata hivyo, NIPASHE ilipomtafuta Chenge kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo, hakupokea simu yake ya mkononi.

No comments:

Post a Comment