Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva.
Kauli ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kwamba kuna uwezekano wa kufanyika kwa pamoja kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu wa mwaka huu, limepingwa vikali na watu wa kada mbalimbali.
Miongoni mwao wamo wasomi, wanasiasa na wanaharakati, ambao wengi
wameonya kuwa, iwapo itatekelezwa kutawakanganya na kuwavuruga wananchi
na hatimaye kuzua vurugu na machafuko nchini.
Walitoa maoni hayo katika mahojiano na NIPASHE yaliyofanyika kwa
nyakati tofauti mikoa kadhaa nchini jana kufuatia kauli ya Mwenyekiti wa
Nec, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, katika mahojiano na gazeti moja la
kila siku nchini
Jumanne wiki hii.
MHADHIRI: ITAWAVURUGA WAPIGAKURA IRINGA
Mhadhiri Msaidizi wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii ya Chuo
Kikuu cha Iringa (UoI), Emanuel Damalo, alisema hoja hiyo ya Nec inaweza
kuvuruga akili za wapigakura kwa kuwa itawalazimisha wafanye maamuzi
yenye ukakasi.
“Huko ni kuwalazimisha Watanzania wapige kura ya maoni bila ya
kutafakari na kufanya uamuzi sahihi. Kauli ya Lubuva (Mwenyekiti wa Nec)
inaashiria kwamba, huo ndio uamuzi wa serikali na alichokifanya ni
kudokeza ili kupima upepo wa kisiasa; kitu ambacho hakiwezekani kwa
sasa,” alisema Damalo.
‘KUNA AJENDA YA SIRI’
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo-Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi, alisema Nec inachopaswa
kusisitiza kwa sasa ni juu ya uandikishaji wa Daftari la Kudumu la
Wapigakura na siyo kuzungumzia kura ya maoni kwa kuwa inadhihirisha kuna
ajenda ya siri nyuma ya kauli yake.
“Niseme kwamba, Nec wasijidanganye wataunganisha kura ya maoni ya
katiba na uchaguzi mkuu na Watanzania wakakubali na kwenda kutekeleza
jukumu hilo kwenye masanduku ya kura. La! hasha! Tutaipinga. Kwa sababu
wanachotaka kukifanya ni kuusukuma umma ukibebe Chama Cha Mapinduzi
(CCM) katika chaguzi ili kisianguke madarakani,” alisema Ole Sosopi.
PROF. NKYA: HOJA YA NEC NI DHAIFU
Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba na Sayansi ya
Jamii cha KCMC, Prof. Watoki Nkya, alisema hoja ya Nec haiwezi
kuushawishi umma kwa sasa kuafiki kuunganishwa kwa mambo hayo mawili,
wakati katiba ni tukio muhimu la kihistoria litakaloliongoza taifa kwa
zaidi ya miaka 50 baadaye.
STOLLA: HAIWEZEKANI KUUNGANISHA MASUALA MAWILI
Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki, Francis
Stolla alisema haiwezekani kuyaunganisha masuala yote mawili kwa wakati
mmoja, kwani yatawachanganya wananchi, ambao hawajawahi kukutana na
jambo kama hilo tangu jadi yao.
Stolla ambaye aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria cha
Tanganyika (TLS), alisema utekelezaji na usimamizi wa mambo yote mawili
ni mgumu, kwani wakati wa uchaguzi kunakuwapo na mambo mengi, ukiwamo
ucheleweshwaji wa vifaa vya kupigia kura katika baadhi ya vituo.
Hivyo, alipendekeza kumalizika kwanza kwa suala la uchaguzi mkuu na
baada ya wananchi kupumzisha akili zao, ndipo kufuatiwe na suala la
kura ya maoni kwa katiba inayopendekezwa.
WASOMI MBEYA WAPINGA
Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasomi Mkoa wa Mbeya, Mzee Prince
Mwaihojo, alisema hatua ya Nec kufikiria kuendesha kura ya maoni
sambamba na uchaguzi mkuu haifai, kwani inaweza kusababisha madhara
makubwa kwa jamii.
“Tukifikiri mambo kwa kina tunaona kwamba, Nec inataka kuwaondoa
wananchi kwenye uchaguzi mkuu ili wajikite kwenye katiba. Hali hiyo
haifai kabisa kwa sababu wananchi watajikuta wakifanya mambo yote
mawili, huku fikra zao zikiwaza jambo moja. Matokeo yake suala mojawapo
halitafanyika kwa ufanisi,” alisema Mzee Mwaihojo.
WAKILI SHITAMBALA: ITALETA MFARAKANO
Wakili wa Kujitegemea na mwanasiasa mzoefu mkoani Mbeya, Sambwee
Shitambala alisema yeye siyo shabiki wa kuona kura ya maoni inafanyika
siku moja na uchaguzi mkuu kwa sababu ana amini huo utakuwa ni mchakato
wenye mfarakano.
Alisema Nec imekuwa haiaminiki, kuanzia matamshi yake mpaka matendo yake, jambo ambalo linawawia vigumu Watanzania kuiamini.
Shitambala ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya,
alipendekeza kuwa kabla ya kufikiria ni lini kura ya maoni itapigwa,
kwanza Nec ielekeze nguvu zake katika kukamilisha uandikishaji wa
wapigakura.
MWANAFUNZI TEKU: NI VIGUMU
Mwanafunzi wa sheria mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Teofilo
Kisanji (Teku) cha jijini Mbeya, Samwel Jonathan, alisema ni vigumu kwa
Nec kuendesha kura ya maoni siku moja na uchaguzi mkuu kutokana na tume
yenyewe kutokuwa na umakini, rasilimali za kutosha na kuingiliwa na
viongozi wa serikali kila wakati.
Alisema ikiwa uchaguzi mkuu wenyewe huitoa jasho Nec kiasi cha
kuonyesha upungufu mkubwa katika baadhi ya maeneo, siyo rahisi kwa tume
hiyo hiyo kufanya kazi zote mbili kwa wakati mmoja na ikafanikiwa.
LOISULIE: ITALETA MKANGANYIKO
Mwenyekiti wa Jumuiya za Wanataaluma Tanzania (ASAs) Paul Loisulie,
alisema ni matukio mawili yenye uzito mkubwa kwa taifa, hivyo
havihitaji kuchanganywa.
“Jaribio lolote la kuchanganya hivi viwili ni kudharau uzito wa
masuala haya. Na athari ni pamoja na kukosesha wananchi fursa ya
kufuatilia kila tukio na kujenga uelewa, hasa katiba inayopendekezwa,”
alisema Loisulie.
CHACHA: KURA YA MAONI ISOGEZWE MBELE
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanataaluma katika Chuo Kikuu cha Dodoma
(Udomasa), Nashon Chacha, alishauri Nec kutokaribisha wazo la kuahirisha
uchaguzi au kuchanganya kura ya maoni ya katiba mpya na uchaguzi kwa
madai muda hautoshi.
KABUTARI: NI KULIPASUA TAIFA
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Kayumbo
Kabutari, alisema lengo la kura ya maoni lililokuwa kupata katiba mpya
itakayotumika kwenye uchaguzi mkuu 2015 limeshindikana, hivyo hakuna
haja ya kulipasua taifa.
NYAMBABE: NI MKAKATI KUIBA KURA
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, alisema huo
ni mkakati, ambao umepangwa kwa ajili ya kuwaibia Watanzania kura.
Alisema wanataka kufanya hivyo ili kuwapumbaza Watanzania waegemee
zaidi katika kitu kimoja ili wao wapate mwanya wa kuiba kura.
Nyambabe alisema hata wakifanya hivyo watakuwa wamekiuka sheria ya
kura ya maoni, ambayo inabainisha kwamba, kabla ya kufanyika kura hiyo,
ni lazima wananchi waandikishwe kwenye daftari ambalo mpaka sasa halipo
na kutolewa kwa elimu ya uraia na mwezi mmoja wa kampeni.
MWAKAGENDA: ITASABABISHA VURUGU
Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) limesema kufanyika kwa kura ya
maoni pamoja na uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu ni uvunjifu wa sheria na
kunaweza kusababisha vurugu kubwa wakati wa michakato hiyo.
Kaimu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda, alisema kura ya
maoni na uchaguzi mkuu vina sheria mbili tofauti, hivyo hatua hiyo
itawachanganya wananchi.
WASOMI: ITAZUA VURUGU
Mmoja wa wasomi kutoka Chuo Kikuu Huria (OUT), Aziz Habibu, alisema
uamuzi wa kuunganisha vitu viwili kwa pamoja unaweza kutoa nafasi ya
kuwapo kwa vurugu kwa kuwa unashirikisha vitu viwili kwa wakati mmoja.
Alisema tayari mchakato wa kura ya maoni ulishaingia dosari katika
eneo lililofanyiwa majaribio, hivyo kuunganishwa na uchaguzi mkuu
kunaweza kusababisha kuwapo kwa uvunjifu wa amani.
Barnabas Kasera kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua)
alisema amestushwa na maamuzi ya Nec kwa kuwa tayari mchakato wa kura ya
maoni umeshashindikana kutokana na mfumo unaotumiwa kusuasua kutokana
na uchache wa mashine.
Joel Mlambiti kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema ameshangazwa na
Nec kuendelea kung’ang’ania kura ya maoni wakati tayari mchakato wa
majaribio ulishashindikana kutokana na ufinyu wa vifaa.
Alisema uchaguzi mkuu mara zote huwa na mambo mengi, ikiwamo
yanayohusu vyama vya siasa kufanya kampeni na kwamba wakati mwingine
kumekuwapo na maeneo ambayo yamekuwa na uvunjifu wa amani.
MGAYA: NI KUWAKOROGA WANANCHI
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania
(Tucta), Nicholaus Mgaya, alisema kufanyika kwa pamoja kura ya maoni ya
katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu ni kuwachanganya wananchi kwa
sababu kila jambo lina ukubwa wake na umuhimu wake.
“Siyo sawa kuwapigisha kura mbili Watanzania; ya katiba na uchaguzi
mkuu, hasa ikizingatiwa kuwa mambo yote haya ni muhimu kwa taifa letu.
Ni vyema likafanyika jambo moja kwanza la uchaguzi ndipo lifuate la
katiba ili Watanzania wapate muda wa kuisoma na kuichambua,” alisema
Mgaya.
POLEPOLE: NI VITU TOFAUTI
Aliyekuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Humphrey Polepole, alisema kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa na
ile ya uchaguzi mkuu ni vitu viwili, ambavyo haviwezi kuchanganywa.
Alisema mchakato wa kupiga kura katika uchaguzi mkuu ni tendo la
kisiasa, ambalo litakwenda kuwapata wabunge, madiwani na rais, lakini
kitendo cha kupiga kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa ni cha
kisiasa, lakini halihusishi vyama vya siasa.
Alisema vyama vya siasa pindi vinapofarakana hukimbilia kupata
muafaka, hivyo mchakato wa katiba inayopendekezwa ukijumuishwa katika
mchakato wa uchaguzi mkuu, utawapa mwanya wanasiasa kuingiza mambo yao
yatakayowasaidia.
“Ni mwiko kuingiza siasa katika katiba. Tukifanya hivyo tutageuza mchakato kuwa agenda ya kisiasa,” alisema Polepole.
Aliishauri Nec kuwa mwaka huu ni ngumu kupata katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba.
Hivyo, alilishauri Bunge kuifanyia marekebisho katiba ya mwaka 1977
ili itumike katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
HELLEN KIJO-BISIMBA: HAIWEZEKANI
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema kufanya kwa pamoja upigaji kura ya
maoni ya katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu haiwezekani kwa kuwa
kila jambo linatakiwa kupewa nafasi yake kutokana na umuhimu wake kwa
taifa.
Alisema michakato yote miwili ikifanyika kwa pamoja itachanganya
wananchi, hasa kutokana na ugeni wa kura ya maoni ya katiba na
kusisitiza bado elimu haijatolewa kwa makundi husika kuyawezesha kufanya
uamuzi sahihi.
“Katiba inayaopendekezwa na uchaguzi mkuu ni vitu viwili tofauti
vikichanganywa, vitaleta mkanganyiko kwa wananchi sababu ya uelewa mdogo
walionao. Ni bora kila jambo likapewa nafasi yake,” alisema Dk.
Bisimba.
Alishauri kuwa ni bora mchakato wa kura ya maoni ya katiba
inayopendekezwa ukaahirishwa mpaka mwishoni mwa mwakani wakati nchi
itakuwa imepata viongozi wapya watakaofanya mipango ya kutoa elimu
ipasavyo na kulisaidia taifa kupata katiba inayotokana na maoni ya
wananchi.
DK. BANA: VITENGANISHWE KWA MUDA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitengo cha
Sayansi ya Jamii, Dk. Benson Bana, alisema kura ya maoni kwa katiba
inayopendekezwa na uchaguzi mkuu haviwezi kwenda pamoja, ila vinaweza
kutenganishwa kwa muda mfupi.
Alisema kwa kuiga mfano wa Zanzibar, ambao mwaka 2010 walifanya
kura ya maoni Julai na uchaguzi mkuu Oktoba, hivyo kura ya maoni inaweza
kufanyika Agosti na uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu.
Dk. Bana alisema ni suala la makubaliano ili kumfanya Rais Kikwete,
ambaye ndiye aliyeanzisha mchakato huo kuondoka madarakani akiwa
amemaliza kuliko kubebesha zigo hilo kwa kiongozi mwingine ajaye.
Imeandkwa na Godfrey Mushi, Moshi; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Ashton
Balaigwa, Morogoro; Augusta Njoji, Dodoma; Isaya Kisimbilu, Elizabeth
Zaya, Christina Mwakangale, Mary Geofrey, Enles Mbegalo, Gwamaka
Alipipi, Salome Kitomari na Hussein Ndubikile, Dar.
No comments:
Post a Comment