Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara 24 tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo 1965.
Dar es Salaam. Vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga huenda wakatangaza
ubingwa Jumatatu ijayo kama watashinda michezo yake mitatu wiki hii
dhidi ya Stand United, Polisi Morogoro na Ruvu Shooting.
Mabingwa mara 24, Yanga baada ya kulazimishwa sare
ya bao 1-1 na Etoile du Sahel Jumamosi katika mchezo wa Kombe la
Shirikisho, wanahitaji ushindi dhidi ya Stand United leo kabla ya
kuivaa Polisi Morogoro Ijumaa na kumalizia na Ruvu Shooting Jumatatu
ijayo.
Yanga sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 46, kama
itashinda mechi tatu hizo kati ya tano itafikisha pointi 55 ambazo
haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwani hata mabingwa watetezi Azam walio
nafasi ya pili na pointi 42 kama itashinda michezo yake minne
iliyobakia itafikisha pointi 54.
Pamoja na ratiba hiyo nyepesi kwa Yanga, kizingiti
pekee kwao kwa sasa ni wimbi la majeruhi linaloiandama timu hiyo baada
ya mabeki wawili wa kati Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani
kuikosa mechi ya leo dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Nahodha Haroub ‘Cannavaro na Yondani waliumia
katika mchezo dhidi ya Etoile du Sahel pamoja na Salum Telela wote
jana walishindwa kufanya mazoezi na wenzao.
Daktari wa Yanga, Juma Sufiani aliliambia gazeti
hili kuwa Cannavaro, Telela na Yondani hawatacheza mchezo wa leo
kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ya vifundo vya miguu.
“Walikuwapo mazoezini ila hawakufanya na wenzao,
Telela na Cannavaro tumewapeleka kufanyiwa vipimo na majibu yataletwa
kesho (leo) ili tujue hali zao zinaendeleaje,” alisema Dk. Sufiani.
Kutokana na majeruhi hayo kocha wa Yanga, Hans
Pluijm atalazimika kumtumia Mbuyu Twite na Rajab Zahiri kucheza beki ya
kati katika mechi ya leo kuziba mapengo ya Yondani na Cannavaro, wakati
Said Makapu atacheza kama kiungo mkabaji akisaidiana na Hassan Dilunga
na Haruna Niyonzima kuziba pengo la Telela.
Kocha Pluijm alisema wanasau kwa muda mambo ya
Kombe la Shirikisho na wanaingia kwenye ligi kusaka ubingwa tu na
watahakikisha wanapambana vilivyo ili kushinda michezo yote iliyobakia.
“Sasa tuna mawazo ya ubingwa tu, tunajua kuwa
mechi na Stand United itakuwa ngumu kwani kila timu tunayokutana nayo
imejiandaa, lakini tumedhamiria kupambana na kuhakikisha tunashinda
michezo yetu mitatu mfululizo ili tuchukue ubingwa mapema,”alisema
Pluijm.
Kocha Msaidizi wa Stand United, Athuman Bilal alisema wamejiandaa vizuri kuikabili Yanga huku akidai hawaihofii hata kidogo.
“Tunaichukulia Yanga kama timu ya kawaida,
wachezaji ni wale wale, viwango vyao havijabadilika, ila tu nikiri
Yanga morali iko juu hivi sasa,” alisema Bilal.
Mshambuliaji tegemeo wa Stand United, Mnigeria Abaslim
Chidiebele alisema alikuwa anaisubiri Yanga kwa hamu ili kutimiza lengo
lake la kuzifunga timu kongwe nchini.
Chidiebele alisema hajawahi kucheza kwenye Uwanja
wa Taifa hivyo anataka kuweka historia kwa kuifunga Yanga kama
alivyofanya dhidi ya Simba mjini Shinyanga.
“Hao mabeki ni majina tu lakini uwezo ni ule ule
kama mabeki wengine, nitapambana mpaka nihakikishe nimefunga bao zaidi
ya mbili nataka kufanya hivyo kwa kuwa ndio mara yangu ya kwanza kucheza
ndani ya nyasi za Uwanja wa Taifa,”alisema Chidiebele ambaye amefunga
mabao tisa msimu huu.
No comments:
Post a Comment