Baadhi ya wananchi wakishiriki upigaji kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Desemba mwaka jana . Picha ya Maktaba
Ilichukua miezi mitano kumaliza mvutano wa kimahesabu na maneno
baina ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Serikali na wadau wa
demokrasia kuhusu muda wa maandalizi na upigiaji Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa.
Kwa miezi hiyo yote tangu Rais Jakaya Kikwete
alivyotangaza Oktoba, 2014 kuwa kura hiyo ingefanyika Aprili 30 mwaka
huu, vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na wananchi
walipinga na kuomba iahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu.
Mbali na hoja ya kutaka shughuli hiyo ifanywe bila
presha, bado kusuasua kwa uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga
kura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR),
kulizidi kuonyesha hesabu za wazi kwamba isingewezekana.
Hata hivyo, Serikali na Nec walisisitiza tarehe
hiyo inayodaiwa kutangazwa na Rais Kikwete kinyume na Sheria ya Kura ya
Maoni 2014. Uamuzi wa Nec kuahirisha zoezi hilo hadi litakapotangazwa
tena kwa mashauriano na Tume ya Uchaguzi Zanzibar, umeleta ushindi kwa
wakosoaji hao.
Uhuru wa Nec shakani
Asilimia kubwa ya wakosoaji wanasema kuwa kitendo
cha Nec kung’ang’ania kisichowezekana ni uthibitisho haina uhuru. Uhuru
huo, kwa mujibu wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard
Mbunda, ulijidhihirisha baada ya tume hiyo kushindwa kujiendesha katika
uamuzi na mipango.
“Kuahirishwa kwa Kura ya Maoni ni kitu
kilichotarajiwa kwa sababu tarehe iliyopangwa isingeweza kufikiwa
kirahisi na aliyeitangaza haikuwa Nec.
“Hii inatufunza taasisi lukuki za umma
hazijiendeshi kiweledi. Zilitakiwa kujiendesha kwa taratibu na
kuwajibika ili kila tamko litekelezeke na siyo kubadili kama
ilivyotokea,” anasema Mbunda.
Hoja ya Uhuru wa Nec isingevuma iwapo ingenyooshea mikono zoezi hilo mapema kutokana na kusuasua kwa uandikishaji kwa BVR.
Licha ya kujua kuwa muda huo usingewezekana, Nec
iliendelea kuubeba mzigo huo mzito ambao mara kwa mara Jaji Lubuva
alikuwa akisisitiza yeye ni ‘Mnyamwezi’ mbebaji wa mzigo mzito na kwamba
iwapo ungemshinda angesema kama alivyofanya Aprili, 2.
Wadau wamemlalamikia Rais Kikwete kwa kuvunja
Sheria ya Kura ya Maoni kwa kutangaza tarehe badala ya muda kama sheria
inavyomtaka na kuwaachia kibarua kizito Nec kukabiliana na
kisichowezekana.
Mwanasheria Halord Sungusia anasema kitendo cha
kuahirisha tarehe ya Kura ya Maoni, kinadhihirisha nguvu ya kisheria ya
Nec juu ya tukio hilo la mwisho la Katiba Mpya.
“Nec imefanya jambo zuri kwa sababu hayo ndiyo mamlaka
iliyopatiwa kisheria. Kwa bahati mbaya yalipokwa na Rais. Kifungu cha
tano cha Sheria ya Kura ya Maoni kinaipa Nec nguvu ya kutangaza tarehe
mahususi ya kura wakati Rais anatakiwa tu kutangaza muda,” anasema
Sungusia.
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, Rais hakuwa amevunja
sheria yoyote na kwamba alifanya hivyo “in the Spirit of law” (ndani ya
dhamira ya sheria) kwa kuwa kifungu namba nne cha sheria hiyo kinampa
madaraka hayo japo tarehe ya kutangaza ni yao.
Jaji Lubuva katika mkutano wake na Waandishi wa
Habari hivi karibuni alisema tume yake ipo huru kama ilivyoanzishwa na
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya 1977 na kwamba yeye,
Makamishna au Wakurugenzi wake hawajawahi kuingiliwa kiutendaji.
“Kumekuwa na dhana kuwa tume yetu haipo huru kwa
sababu viongozi wanateuliwa na Rais na sisi kwenye Katiba Mpya
tulipendekeza mabadiliko. Sasa tukiacha shughuli kwa sababu ya dhana
hiyo, mambo hayataenda. Ila ikitokea imeamuliwa waje wengine sisi
tutaondoka,” anasema Jaji Lubuva.
Kuahirishwa kwa Kura ya Maoni ni matokeo ya
mwenendo mbovu wa uandikishaji wapigakura kwa BVR ambao umegubikwa na
ukata wa kibajeti.
Nec ilijikuta katika wakati mgumu tangu awali
baada ya idadi ya mashine walizokuwa wakihitaji kuendelea kupunguzwa
kutoka 15,000 hadi 10,500 na baadaye idadi ya sasa mashine 8,000.
CCM inahusika na yaliyotokea
“Tume inaonekana wazi kuwa haikuwa huru. Ilisema
kabisa haina vifaa vya kutosha lakini iliendelea kulazimisha kuwa Kura
ya Maoni ingefanyikakwa tarehe iliyopangwa. “Hata mtu ambaye hajasoma
hesabu alikuwa anajua kuwa isingewekana kura hiyo kupigwa Aprili, 30,”
anasema Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa, Isaiah Salmon. Anasema tamko la
Rais Kikwete juu ya tarehe hiyo lililenga kuwapumbaza wananchi ili CCM
ijiandae na Uchaguzi Mkuu na ulazimishaji huo ulifanywa kwa makusudi kwa
masilahi ya kisiasa.
‘Ujanjaujanja huo, anasema utaathiri imani ya
wananchi kwa Rais Kikwete na serikali yake kuwa huenda kuna mambo mengi
hufanywa kwa presha,” anasema Salmon.
Iwapo kulazimishwa kwa Kura ya Maoni kulifanywa
kwa masilahi ya CCM na Serikali inakosa uhakika kutokana na Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kusema chama chake hakihusiki na
‘uzembe’ huo.
“CCM hatuhusiki na haihitaji kwenda shule kujua
kuwa tangu awali mambo hayakuwa mazuri. Kimsingi hawa watu (Nec) lazima
wawajibike…ikifikia mahala umeshindwa, wajibika.“Lazima tuseme wazi hii
ni nyeupe na hii ni nyeusi,” anasema Nape.Nape anaenda mbali na
kuwatuhumu viongozi wa Nec kwamba walipanga ‘kupiga pesa’ kwa vikao na
semina” huku akimtetea Rais Kikwete kwa kusema “siamini kama Rais
alitangaza bila kupata ushauri wa tume. Naamini kulikuwa na mawasiliano
baina yao.
No comments:
Post a Comment