Arusha/Mtwara. Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), kimetangaza mkakati wake katika Uchaguzi Mkuu kwa
Mkoa wa Arusha, lengo likiwa ni kuzoa majimbo na kata zote.
Mwenyekiti wa madiwani wa chama hicho mkoani
Arusha, Isaya Doita alisema jana kuwa: “Tunakusudia kutumia chopa tano
Kanda ya Kaskazini, magari ya kisasa ya kampeni yenye uwezo wa kuendesha
mikutano mikubwa ya hadhara mwaka huu.”
Alisema Chadema Kanda ya Kaskazini kwa
kushirikiana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamejipanga
kushinda majimbo yote 33 na kata 673 ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na
Manyara.
Doita alisema katika kuhakikisha ushindi
unapatikana wamejipanga kuwakutanisha wagombea wote wa udiwani na
ubunge ili kuweka mikakati ya kampeni hizo.
“Ukombozi una gharama zake, sisi tunaomba tushirikiane kwa kuchangiana ili kuhakikisha Watanzania wanakuwa huru,” alisema Doita.
Katika hatua nyingine, Chadema imeitaka Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuweka wazi tarehe za kuanza uandikishaji wa
wapigakura mkoani Mtwara.
Uandikishaji wa wapigakura kwa sasa unaendelea katika miji na vitongoji vya Mkoa wa Njombe.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika
alisema maelekezo ya NEC ni kwamba baada ya Njombe ni Mtwara, lakini
haijaweka bayana tarehe, mji wala kitongoji kitakachoanza uandikishaji.
Mnyika aliwataka wananchi wa Mtwara kujitokeza kwa wingi wakati uandikishaji utakapokuwa mkoani humo.
Alisema chama chake kinaazimia kuifanya Lindi na
Mtwara kuwa Kanda ya Kusini wakati Ruvuma itakuwa katika Kanda ya Nyanda
za Juu Kusini kiutendaji.
No comments:
Post a Comment