Mara kadhaa viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakiwaonya wanachama wao dhidi ya makada wanaotumia fedha kujitengenezea mazingira mazuri ya kupitishwa na chama hicho kugombea urais, lakini wameeleza kuwa hawawajibiki kuwaripoti Takukuru kwa kuwa ni wajibu wa chombo hicho cha kuzuia na kupambana na rushwa kufanyia kazi malalamiko hayo.
Dar es Salaam. Wakati viongozi wajuu wa CCM wakiendelea
kulalamikia makada wanaowatuhumu kutumia fedha kujifagilia njia ya
urais, mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah amesema taasisi yake
inakusanya taarifa zote za wanachama wa chama hicho tawala wanaotuhumiwa
kutumia mlungula.
Mara kadhaa viongozi wa juu wa CCM wamekuwa
wakiwaonya wanachama wao dhidi ya makada wanaotumia fedha kujitengenezea
mazingira mazuri ya kupitishwa na chama hicho kugombea urais, lakini
wameeleza kuwa hawawajibiki kuwaripoti Takukuru kwa kuwa ni wajibu wa
chombo hicho cha kuzuia na kupambana na rushwa kufanyia kazi malalamiko
hayo.
Jumatano, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alisema Takukuru hawahitaji kupata
mwaliko wa CCM ili kufanya uchunguzi wa kukamata wagombea wanaotumia
rushwa ndani ya chama hicho kwani rushwa inayoendelea kwa sasa iko wazi.
“Kazi ya kuwafuatilia imeshaanza muda mrefu,
tunazo taarifa zao za kutosha kwa kila mwanasiasa anayelalamikiwa,”
alisema Dk Hoseah wakati alipoongea na gazeti hili kuhusu sababu za
taasisi yake kukaa kimya wakati ikielezwa hadharani kuwa rushwa imezidi
katika harakati za uchaguzi ndani ya CCM
Dk Hoseah alisema kwa muda mrefu Takukuru imekuwa
ikifuatilia mienendo ya wanasiasa wanaotaka uongozi kupitia chama hicho
na ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema Takukuru kwa sasa inaendelea na kazi yake
ya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo huku ikikusanya taarifa za kila
mwanasiasa anayeonekana kutuhumiwa na vitendo vya rushwa.
“Siyo kwamba Takukuru haijaona wala haisikii
malalamiko ya viongozi CCM. Tunajua wajibu wetu na kazi ya kuwafuatilia
imeshaanza,” alisema Dk Hoseah.
“Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010
imekataza wazi kwamba, ni makosa kutoa chochote kama zawadi kwa kundi la
watu, vinginevyo ni kukiuka sheria hiyo. Labda kama anaonekana kuwa na
fedha nyingi basi ajenge hata barabara kuliko kufanya hivyo.”
Dk Hoseah aliongeza kuwa sheria pia inazuia kuanza
kampeni kabla ya muda kupangwa rasmi na Tume ya Taifa (Nec), kwa hivyo
muda wa kampeni utakapoanza, itarahisisha kukusanya taarifa zake na
kuchukua hatua kwa wanasiasa hao.
“Kwanza ni kosa kufanya kampeni kabla ya muda,
lakini pia ni kosa kutoa zawadi kama maji ya kunywa kama unafahamu kuwa
wewe ni mwanasiasa utakayegombea. Sheria yetu ya Takukuru inaweka wazi
pia kitendo hicho ni kosa,” alisema Dk Hoseah.
Mapema wiki hii, akiwa kwenye vikao vya ndani na
viongozi wa chama hicho wa Dar es Salaam, makamu mwenyekiti wa CCM,
Phillip Mangulla alisema fedha zinazotumiwa na makada kununua wanachama
“kama maandazi”, zitakuwa kitanzi chao kwenye uchaguzi mkuu, akisisitiza
kuwa wanachama hao watang’olewa.
Mbali na Mangula, wengine waliowahi kulalamikia
rushwa ndani ya chama hicho ni mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete ambaye
alitahadharisha kuwa jambo hilo linaweza kukiuangusha chama.
Mangula amtaja mgombea
Wakati Dk Hoseah akisema hayo, Mangulla juzi
alidokeza uwezekano wa chama hicho kuwatema makada sita ambao
wamesimamishwa kujihusisha na uchaguzi kwa mwaka mmoja, akisema kuwa CCM
itampitisha mgombea ambaye “amekidhi vigezo, kanuni na taratibu” zao.
Mangula alisema hayo wakati wa majumuisho ya ziara yake mkoani Dar es Salaam kwa kuongea na viongozi.
“Chama kitafuata taratibu zote husika bila kuwepo
kwa shinikizo kutoka kwa wanaotaka kuwania nafasi hiyo... wanachama
wenye nia ya kugombea nafasi ya urais na nyingine wanapaswa kusubiri
mpaka utaratibu wa kutangaza nia na kufanya kampeni utakapotangazwa kwa
mujibu wa taratibu na kanuni za chama,” alisema Mangula ambaye
alisisitiza wanachama kuepuka makundi ya urais.
Waliopewa adhabu kwa kukiuka taratibu zinazozuia
kuanza kampeni mapema ni Edward Lowassa na Frederick Sumaye, ambao ni
mawaziri wakuu wa zamani, Bernard Membe (waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, January Makamba (Sayansi na Teknolojia),
Steven Wasira (Kilimo na Chakula) na William Ngeleja.
Wafuasi wa wagombea hao wamekuwa wakishambuliana
kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, hali inayoonyesha wazi
kuwapo kwa makundi.
Kutokana na hali hiyo, viongozi wa CCM wametakiwa
kuwachukulia hatua wanachama wanaoeneza siasa za makundi zenye kuzua
migogoro inayotishia umoja na mshikamano ndani ya chama hicho.
Mangula alisema wanachama wa CCM wanapaswa
kufahamu kuwa mgombea atakayesimamishwa ndiye atakaye wakilisha chama na
si kujiwakilisha yeye, hivyo wanapaswa kumuunga mkono.
No comments:
Post a Comment