Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara imesema kuwa itawachukulia hatua kali za kisheria wasimamizi wa vituo vya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura ikiwa watafanya upendeleo uandikishaji utakapoanza wilayani humo.
Onyo hilo lilitolewa jana wilayani hapa na Kamanda wa Taasisi hiyo,
Nestory Gatahua, alipokuwa akizungumza na wasimamizi hao kwenye mafunzo
ya uadikishaji wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa
wasimamizi hao wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi mjini hapa.
Alisema jukumu hilo ni la serikali, hivyo linapaswa kupewa umuhimu
wake katika usimamizi na utekelezaji ili lifanyike kwa hali ya umakini
wa hali ya juu na kufikia lengo la uandikishaji.
Gatahua alisema Takukuru itafuatilia kwa ukaribu uandikishaji
katika kila kituo ili kuangalia mwenendo mzima wa uandikishaji
utakapoanza wilayani humo na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya
msimamizi yeyote atakayebainika kwa kosa la kupokea rushwa ama kutumia
vibaya fomu za uandikishaji kwa maslahi yake binafsi.
“Msimamizi wa kituo anapaswa kutambua umuhimu wa zoezi hili…
Taasisi yetu itafuatilia kwa karibu zoezi la uandikishaji kuanzia mwanzo
hadi mwisho na iwapo msimamizi atabainika kitendo cha rushwa
atawajibishwa kisheria,” alisema Gatahua.
Alisema uandikishaji wa uboreshaji wa daftari la kudumu la
wapigakura sio mchakato wa kisiasa, hivyo kama msimamizi yeyote atakuwa
na itikadi ya vyama kwa kutoa upendeleo katika uandikishaji kwa
kuangalia vyama vya siasa ni kinyume cha sheria, hivyo Takukuru
inawajibika kumchukulia hatua msimamizi wa aina hiyo.
Kamanda huyo alisisitiza kuwa namba za simu za Taasisi hiyo
alizotoa kwa wasimamizi hao wazifanyie kazi na kila msimamizi awe mlinzi
wa mwenzake atakapomuona anakwenda kinyume cha kiapo cha utiifu kwa
lengo la kuhakikisha jukumu hilo linatekelezwa kikamilifu.
Gatahua aliongeza kuwa wasimamizi hao wasitishwe na viongozi wa
vyama vya siasa, badala yake wanatakiwa kufuata sheria na kanuni za
mafunzo hayo waliyoyapata kutoka kwa wawezesheji hao kwani ulinzi wa
kutosha upo, hivyo hawana sababu ya kuharibu kazi waliyopewa.
No comments:
Post a Comment