Monday, 27 April 2015

Mahakama ya Kadhi sasa yamtisha Mrema.


Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Agustino Mrema.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Agustino Mrema, amewaonya wanasiasa wanaotumia suala la Mahakama ya Kadhi kumchafua katika jimbo lake la Vunjo na kuwataka viongozi wa dini kuwapuuza kwa kuwa suala hilo liliasisiwa na Chama cha NCCR-Mageuzi na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, alisema suala la Mahakama ya Kadhi liliasisiwa na NCCR Mageuzi mwaka 1995 na kuliingiza katika ilani yake ya uchaguzi na alipohamia chama hicho alilikuta.
 
“Viongozi wa NCCR-Mageuzi wanaenda kunichafua kwenye jimbo langu la Vunjo kwamba mimi ndiye muasisi wa Mahakama ya Kadhi wakati si kweli kwani suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi lilikuwapo kwenye ilani ya uchaguzi ya NCCR-Mageuzi katika ukurasa wa tisa,” alisema.
 
Mrema alimtaja Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi,James Mbatia, kwamba ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamekuwa wakimpiga vita kwa kutumia suala la Mahakama ya Kadhi ili maaskofu, wachungaji na waumuini wa kikristo wamkatae katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
 
Aliongeza kuwa kwa upande CCM kiliingiza suala la kuanzishwa Mahakama ya Kadhi mwaka 2005 katika ilani yake ya uchaguzi.
“CCM na NCCR-Mageuzi wanatumia Mahakama ya Kadhi kunimaliza kisiasa, lakini nahawakikisha wananchi wa Vunjo kwamba suala la mahakama hiyo mimi siyo muasisi   wake   kama   inavyoelezwa.
 
Mbatia,alipoulizwa kuhusiana na madai ya Mrema, alijibu kwa kifupi katika ujumbe wake kwenye simu ya mkononi kwamba amemsamehe Mrema.

No comments:

Post a Comment