Akiwahutubia mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza kwenye Viwanja vya Furahisha juzi, Zitto alisema hawezi kumzuia mtu anayetaka kujiunga ACT - Wazalendo ikiwa atafuata taratibu zilizowekwa na chama hicho.
Mwanza. Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe
amesema iwapo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa anataka kugombea
urais kupitia chama hicho afuate taratibu za chama ikiwamo kutangaza
mali zake.
Akiwahutubia mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza
kwenye Viwanja vya Furahisha juzi, Zitto alisema hawezi kumzuia mtu
anayetaka kujiunga ACT - Wazalendo ikiwa atafuata taratibu zilizowekwa
na chama hicho.
“Naomba niwaambie Watanzania kwamba ACT siyo chama
cha kumtengenezea mtu mazingira ili agombee urais, lakini kama Lowassa
anataka kugombea urais kupitia huku lazima atangaze mali zake na kueleza
wapi amezipata kama taratibu za chama zinavyosema,” alisema Zitto na
kuongeza:
Zimekuwapo taarifa kwenye vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya wagombea akiwamo Lowassa ambaye
anatajwa kuwania urais kupitia CCM, wana mpango wa kutimkia ACT iwapo
watakatwa majina yao katika mchujo wa wagombea.
Kwa mujibu wa habari hizo, ACT - Wazalendo imepewa
fedha na Lowassa ambazo inatumia katika mikutano hiyo kumwandalia
nafasi ya kuwania urais, madai ambayo pande zote zimeyakanusha.
Akizungumzia taarifa hizo kwenye mkutano huo,
Zitto alisema chama chake kinaongozwa kwa kufuata taratibu na kitampokea
yeyote atakayefuata taratibu hizo.
Kiongozi huyo ambaye hivi karibuni alitangaza mali
na madeni yake, alisema iwapo Lowassa atataka kujiunga na chama hicho
itambidi atangaze mali zake na kueleza jinsi alivyozipata, kama yeye
(Zitto) alivyofanya.
Hata hivyo, akizungumzia kuhusu kauli ya Zitto,
msemaji wa Lowassa, Aboubakary Liongo alisema: “Hakipo kitu kama hicho
na hakitakuwapo, hatujui habari hii inatoka wapi? Mzee (Lowassa) amekuwa
akitumikia CCM maisha yake yote tangu enzi za TANU … yupo na anaendelea
kutumikia kifungo chake. Maisha yake yote ni mtumishi wa chama.”
Lowassa pamoja na makada wengine watano wa chama
hicho walipewa adhabu ya onyo kali baada ya Kamati Kuu ya CCM kuwatia
hatiani kwa kuanza kampeni za urais mapema na kukiuka maadili ya chama.
Mbali ya Lowassa, wengine waliofungiwa ni Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja;
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Licha ya muda wa adhabu hiyo kufikia tamati tangu
Februari mwaka huu, chama hicho kilisema kinaendelea kuchunguza mienendo
yao na hakijaeleza hatma yao.
Juzi, gazeti hili liliripoti kuwapo kwa mkakati wa
chama hicho kukata majina ya baadhi ya wagombea wanaoaminika kuwa na
makundi yanayokihatarisha, wakilengwa Lowassa na Membe ili kipitishe
mgombea asiyekuwa na kundi.
Ujumbe kwa Mwigulu
Katika mkutano wake uliofurika wakazi wa Mwanza,
Zitto pia alikanusha madai kwamba amemwandikia ujumbe Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba kwa njia ya barua pepe kuhusu fedha za ziara,
akisema hawezi kufanya hivyo kwamba na hizo ni propaganda za kisiasa.
“Kuhusu mimi kuwasiliana na Mwigulu hizo ni propaganda za kisiasa, siwezi kufanya hivyo kwa mtu ambaye amenikuta bungeni.”
Alisema watu wanaohoji kuhusu ufadhili wa chama
hicho ni vyema kwanza wakajiuliza, Chadema kabla hakijaanza kupata
ruzuku nani alikuwa akikifadhili.
“Ni jambo la ajabu kuona watu wanahoji kuhusu ACT
kufadhiliwa, naomba niwaambie kwamba wawaulize Chadema kabla haijaanza
kupata ruzuku ilikuwa ikifadhiliwa na nani, wamulize Mbowe. ACT ni chama
cha wazalendo hivyo wananchi ndiyo wanakiendesha,” alisema.
Zitto alisema kuna wanasiasa ambao ni wachanga na
amewasaidia kupata ubunge lakini hivi sasa wanamtukana, lakini akasema
watambue kwamba amekwepa mishale mingi na ataendelea kupambana kutetea
masilahi ya wanyonge.
Alisema awali, alipokuwa akipita Ubungo, Kawe,
Singida, Mwanza na majimbo mengine kufanya kampeni kuwasaidia wanasiasa
wa maeneo hayo kupata ubunge, alionekana lulu lakini hivi sasa wanamsema
vibaya.
“Kama mtu ni msaliti kwa nini mnamuita awasaidie
kufanya kampeni, nimekwepa mishale mingi, siasa siyo chuki ni kujibu
hoja, naomba niwaambie kwamba ng’ombe anaweza kutingisha mkia wake
lakini mkia hauwezi kutingisha kiwiliwili chake,” alisema Zitto huku
akishangiliwa.
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mughwira alisema
Mkoa wa Mwanza umepewa kipaumbele na chama hicho, kwani kutakuwa na
ofisi kuu ya chama baada ya Dar es Salaam.... “lakini kama tutachukua
dola tumekusudia kuhakikisha makao makuu ya nchi tunayapeleka Dodoma.”
No comments:
Post a Comment