Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amekanusha madai yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kuandikisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika ngome za CCM na kueleza kuwa huo ni upotoshaji mkubwa kwani Tanzania nzima ni ngome ya chama hicho.
Mbali na hilo amekanusha pia tuhuma zilizotolewa kuwa chama hicho
kinakisaidia Chama cha ACT Wazalendo, akisema hawana sababu ya kufanya
hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, Nape
alisema ratiba ya NEC haijapangwa kimkakati kama alivyodai Dk. Slaa
kwani kila Mtanzania ataandikishwa kwa mujibu wa sheria, hivyo kauli
hiyo ina lengo la kuwapotosha na kuwapa hofu wananchi.
"Kwa kauli hizi ni uthibitisho tosha kuwa wenzetu vyama vya
upinzani hasa Chadema siasa zao zina lengo la kuwagawa watu kikanda,
uthibitisho wa mbegu mbaya ya chuki," alisema na kuongeza:
"CCM wanalaani vikali siasa za namna hiyo kwani siyo hoja za
msingi ila ni za kuwagawa wananchi na kupandikiza chuki zisizokuwa na
maana na suala hilo linaonyesha jinsi wapinzani wanavyofanya siasa za
kikanda."
Nape alisema wapinzani wanajua kuwa watashindwa na CCM ndiyo maana wanafanya fitina na kuwataka kuwagawa wananchi.
Alivitaka vyama vya siasa kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa
wingi kujiandikisha badala ya kueneza upotoshaji na kuwatia hofu zisizo
na msingi kwa wananchi.
Akizungumzia kuhusu ACT Wazalendo, Nape alisema CCM haina sababu
ya kusaidia chama kingine cha siasa hivyo uvumi huo ni uchafuzi wa
kisiasa.
No comments:
Post a Comment