Serikali hii inashangaza. Mwishoni mwa mwaka jana ilipotangaza
kwamba Aprili 30 mwaka huu itakuwa siku ya kupiga Kura ya Maoni kwa
Katiba Inayopendekezwa iliona mbali sana.
Serikali ilielezea ilivyojipanga kuhakikisha Kura
ya Maoni inafanyika kwa ufanisi; kwamba asasi za kutoa elimu
zitaruhusiwa kufanya kazi hiyo na timu za kampeni za NDIYO na HAPANA pia
zingekuwa na muda wa kutosha.
Kwa kuzingatia muda, asasi za kiraia, vyama vya
upinzani na wasomi walionyesha shaka yao juu ya tarehe hiyo kwamba Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) isingeweza kukamilisha uandikishaji mapema na
kusimamia kura hiyo.
NEC ilisita kuwajibu wenye shaka na ilisita
kujifunga kuwa inaweza hadi ilipoahidiwa kupewa mashine za BVR 8,000
kati ya 15,000 ilizoomba kwa ajili ya kuandikisha wapigakura. Hapo ikawa
inasisitiza kuwa itakamilisha kazi hiyo mapema hivyo Kura ya Maoni
itakuwepo kama ilivyopangwa.
Hivi sasa, kila mmoja ni shahidi kwamba mwaka 2014
uliisha bila mashine hizo kuwasili. Kila mmoja ni shahidi pia kwamba
ilipofika Januari hadithi ikawa mashine ziko njiani na hata NEC
ilipoanza kuandikisha wapigakura Februari 23 kwa kutumia BVR 250
ilizokuwa nazo, katika Mkoa wa Njombe, haikupewa mashine za ziada.
Kuona hivyo, NEC, bila aibu,ilikwenda Nigeria na
Kenya kuomba mashine za BVR lakini ilinyimwa. Nigeria walikataa kwa vile
nao walikuwa wanakabiliwa na uchaguzi mkuu Machi 28 huku Kenya wakisema
wanatumia kuboresha daftari lao kila siku.
Aprili 2, NEC ikiwa imeelemewa na mzigo wa lawama
na shutuma, ililazimika kutangaza kuahirishwa kwa Kura ya Maoni hadi
hapo itakapotangazwa tena. Mpaka sasa NEC haijakamilisha uandikishaji
wapigakura Njombe. Je, itamaliza lini nchi nzima kwa ajili ya uchaguzi
mkuu?
Kwa ratiba ya matukio ya mwaka huu – vikao vya
uteuzi wagombea urais, ubunge na udiwani, Bunge la Bajeti, kampeni za
uchaguzi mkuu – hatuoni uwezekano wa kufanyika mwaka huu, labda itokee
miujiza.
Hofu yetu kubwa ni kwamba kusuausua uandikishwaji
wapigakura kulikosababisha Kura ya Maoni kuahirishwa ndiko tunaona
kunajirudia kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 30 mwaka huu.
Serikali inaona ni mbali sana, NEC inaona mbali
sana, chama tawala, CCM, kinaona mbali sana na wafuasi wa chama hicho
wanaona mbali sana.
Je, si kweli kwamba Serikali iliona tarehe ya Kura
ya Maoni iko mbali sana? Je, viongozi wa CCM na NEC si waliona Aprili
30 iko mbali sana? Hadi leo mashine za BVR hazijaongezeka, uandikishaji
tena katika mkoa huo mmoja unakwenda mwendo wa konokono na kuna hatari
tukafika Oktoba watu wengi wakawa hawajapata nafasi ya kuandikishwa.
Tunaamini kusuasua huku si bure. Serikali inajua
kila baada ya miaka mitano unafanyika uchaguzi mkuu mwingine, kwa nini
imesubiri hadi dakika za mwisho ndipo inahamanika kutafuta BVR?
Vilevile, Serikali ndiyo ilitangaza mwaka 2012 kwamba
uandikishaji utakuwa kwa mfumo wa BVR, kwa nini ilisubiri dakika za
mwisho ndipo ianze kukimbia huku na kule kwenda kuazima kutoka nchi
jirani badala ya kununua?
Serikali itafute fedha haraka inunue mashine na
kazi ya uandikishaji ifanyike kama ilivyopangwa ili wananchi watumie
haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi wanaowataka. Hatutapenda
kusikia visingizio vyovyote vikitumika kuathiri uchaguzi mkuu.
No comments:
Post a Comment