Jengo la Makumbusho ya Taifa Mnazi Mmoja, Zanzibar.
Mkurungenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Profesa Audax Mabulla, amesema kuwa kutokana na kuwapo kwa upotoshaji wa mambo ya Muungano, wamefungua milango Makumbusho ya Taifa kwa Watanzania wenye mashaka ili waende kupata usahihi.
Profesa Mabula alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa maonyesho ya maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano.
Onyesho hilo ambalo lilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa
serikali, pia baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi jijini Dar es
Salaam waliopewa mafunzo ya Muungano ya siku tatu kuanzia Aprili 20, ili
wakawe mabalozi kwa wengine.
Profesa Mabula alisema umekuwepo upotoshaji wa mambo ya Muungano
hivyo wameanza kutoa elimu kwa makundi tofauti ili waweze kuuelewa.
“Tumeanzisha ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya ofisi yangu na ya
Makamu wa Rais Muungano ambapo sasa makumbusho tumepata fursa ya kutoa
elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi za mkoa wa Dar es Salaam,
tulikuwa na wanafunzi zaidi ya 3000 ambao wamenufaika,” alisema.
Alisema kupitia watoto hao wanaamini kuwa kizazi chao kitaendeleza mazuri ya Muungano na kuulinda na kuuheshimu.
“Karume na Nyerere walikuwa na busara na akili sana wakauanzisha
kwa kuangalia mahusiano ya Tanganyika na Zanzibar, kiolojia (elimu ya
mambo ya kale) upo ushahidi unaoonyesha visiwa vya Zanzibar na Bara
vilikuwa nchi moja na zipo zana zinazoshabihiana’’ alibainisha.
Pia aliiomba ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, kuendelea kutoa
ushirikiano kwao ili waweze kutoa elimu zaidi hadi mikoani, ombi ambalo
lilikubaliwa na waziri wa ofisi hiyo, Samia Suluhu.
Suluhu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maonyesho hayo kwa upande
wake alisema, baada ya miaka 50 ya Muungano sasa wamefungua ukurasa mpya
kati ya ofisi yake na Makumbusho ya Taifa.
Alisema kwa sasa wametoa nafasi kwa Makumbusho ya Taifa kutoa elimu
ya kuelezea mambo ya Muungano ili Watanzania waweze kuuelewa.
Alisema mwaka uliopita walielekeza elimu hiyo kwa wanavyuo na kutoa
semina mbalimbali kwa wanasiasa, viongozi wa dini na wawakilishi kutoka
pande mbili yaani Zanzibar na Tanzania bara.
Aliwataka wanafunzi waliopata fursa ya elimu hiyo kuwa mabalozi kwa wenzao kwa kusambaza kile walichojifunza.
“Hii ni fursa nzuri kuonyesha ufahamu wetu kwa njia ya picha,
machapisho yaliyoandikwa kutoka mwaka 1964 na kujionea vifaa vya
kihistoria vilivyosababisha tukaungana,” alisema.
Alisema mwaka huu kauli mbiu ina ujumbe usemao, ’Miaka 51 ya
muungano tudumishe amani na muungano na tuipigie kura ya ndio katiba
inayopendekezwa,’
No comments:
Post a Comment