Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Jeshi la Polisi Zanzibar, limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) waliokuwa wakikaidi amri ya kutotoka wilaya moja kwenda nyingine kuhudhuria mkutano wa hadhara. Inakumbukwa kwamba baada ya wafuasi wa CUF kushambuliwa mwishoni wa mwezi uliopita wakitoka katika mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja, polisi waliitisha mkutano nabaadhi ya vyama vya siasa na kupiga marufuku wafuasi kutoka wilaya moja kwenda nyingine.
Hata hivyo, amri hiyo ya polisi inapingwa vikali na viongozi wa
CUF, ambao wameapa kuendelea kusafirisha wafuasi katika kila pembe ya
Zanzibar kuhudhuria mikutano ya hadhara.
Lakini katika kuwadhibiti, polisi juzi waliweka vizuizi kadhaaa
barabarani kuzuia wafuasi waliotoka mjini kwenda kuhudhuria mkutano eneo
la Kilombero, Jimbo la Kitope, linalowakilishwa na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
“Sisi tunataka vyama vya siasa vifuate sheria kwa maslahi ya
usalama wao na nchi. Tumelazimika kutumia mabomu ya machozi
ili kuwatawanya baadhi ya wafuasi wa CUF waliokuwa wameanza kurushia
askari mawe,” alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini, Hasan Msangi.
Askari wa jeshi hilo waliweka ulinzi mkali katika maeneo hayo na
kila mwananchi aliyekuwa akipita, alikuwa akihojiwa na kujieleza
anakoelekea.
Hali hiyo ilikuwa mithili ya mpaka wa Tanzania na nchi jirani kama
Kenya iliyotawaliwa na ulinzi mkali, ndivyo ilivyokuwa juzi Zanzibar
baina ya wilaya na wilaya nyingine.
NIPASHE ilishuhudia kundi la askari polisi wakizuia wimbi la
wafuasi wa CUF waliokuwa wakihudhuria mkutano huo uliohutubiwa na Katibu
Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.
Licha ya jeshi hilo kuweka vizuizi baina ya mpaka wa wilaya ya
Kaskazini ‘B’ na wilaya nyingine, wafuasi wa CUF walitumia njia mbadala
kuhakikisha wanahudhuria mkutano huo na kwa kiasi walifanikiwa.
Wafuasi hao baada ya kutakiwa na jeshi hilo kurudi walikotoka
wakiwa katika magari ndipo walipotumia ujanja wa kupita njia za panya
wakitembea kwa miguu mpaka kufika katika eneo la mkutano, huku
wakiwaacha polisi wakipigwa na mshangao baada ya kuwaona wamefika katika
eneo la mkutano.
Mvua kubwa zilinyesha katika mkutano huo, lakini wafuasi na
viongozi wa CUF hawakujali, badala yake walivumilia kulowa
ili kuhakikisha mkutano huo unamalizika katika muda waliopangiwa.
MAALIM SEIF AHUTUBIA
Maalim Seif akiwahutubia wananchi na wafuasi wa CUF alilaani vikali
kitendo cha jeshi hilo kuweka vizuizi kila pembe ya eneo la mkoa huo
ili wananchi washindwe kuhudhuria mkutano huo.
“Mimi siwalaumu hawa askari waliowekwa katika mipaka baina ya
Wilaya ya Kaskazini B na wilaya nyingine. Hawa wamepewa amri,
wanatekeleza. Mimi nawalaumu viongozi wao, akiwamo Kamishna wa Polisi
Zanzibar, ambaye ndiye aliyewaamrisha,” alisema Maalim Seif.
Alilitaka jeshi hilo kutoa ufafanuzi juu ya sheria waliyotumia
kuwazuwia wananchi kuhudhuria katika mikutano kutoka wilaya moja kwenda
nyingine akisema kitendo hicho kinazuia uhuru wa watu kushiriki shughuli
za kisiasa.
Pia alilishauri jeshi hilo kuzingatia hali ya uchumi na mazingira
ya Zanzibar, kwani kitendo cha kuweka vizuizi barabarani
kinaleta taswira mbaya kwa wageni na kinaweza kuathiri hali ya uchumi
ikizingatiwa kuwa Zanzibar inategemea zaidi sekta ya utalii.
Maalim Seif alisema CUF imekuwa ikipigania maslahi ya Zanzibar, ili kujikwamua kisiasa na kiuchumi.
Alisema katika jitihada za kuwakwamua wananchi kiuchumi, CUF
inakusudia kutekeleza kwa vitendo sera ya bandari huru, jambo ambalo
litaongeza ajira kwa vijana na hatimaye kunyanyua kipato cha wananchi.
Sambamba na hilo, Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Zanzibar, alisema lengo la CUF ni kuhakikisha inajenga mazingira
na miundombinu imara ili kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali,
zikiwamo utalii na uvuvi wa bahari kuu.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema
wanapinga kwa nguvu zote kitendo cha kunyimwa uhuru wao wa kikatiba kwa
kuzuiwa kuhudhuria mkutano wa chama hicho kutoka wilaya moja kwenda
nyingine.
“Polisi waache kuvunja Katiba ya Zanzibar kwa kuwaadhibu wafuasi wa
CUF kuhudhuria mikutano yao ya hadhara. Haiwezekani kuwazuia wanachama.
Hili jambo halikubaliki, halikubaliki, halikubaliki,” alisema Mazrui.
Alisema Zanzibar kuna tatizo la uhasidi kutokana na kuwapo kwa
kundi la vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaojifunza uharamia kwa
kuwadhuru Wazanzibari wezao, ambao ni wafuasi wa CUF.
Mjumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Edi Riyami, alisema
wananchi wa Zanzibar wameanza kuvunjika moyo kuhusiana na mfumo wa
serikali ya Umoja wa Kitaifa kutokana na vizuizi wanavyowekewa na jeshi
hilo.
Alimtaka Maalim Seif kuwapa uhakika Wazanzibari mustakabali wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Mnapotuwekea vizuizi vya kuhudhuria mkutano mnamaanisha nini na
wewe umo Maalim Seif, kwa sababu wewe pia umo katika serikali hii.
Tuliyoipigia kura kwa pamoja sasa tumeanza kupoteza dira ya
kutoaminiana,” alisema Riyami.
Alisema licha vya viashiria vya uvunjifu wa amani vilivyotokea
Zanzibar, hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya serikali iliyotoka kulaani
vitendo hivyo.
Riyami aisema wananchi wa Zanzibar hawataki kuiona hali hiyo
inaendelea Zanzibar kwa jeshi hilo kuweka vizuizi na kumtaka Maalim Seif
kwenda katika Serikali ya Jamuhuri ya Muungano kupinga vizuizi vya
jeshi, ambalo ni sehemu ya serikali hiyo.
Baada ya mkutano huo kumalizika, Maalim Seif alihakikisha watu wote
wanaondoka katika eneo la mkutano ndipo na yeye alipoondoka akihofia
wafuasi wake kupigwa na askari wa jeshi hilo kutokana na mazingira
kutokuwa rafiki baina ya jeshi hilo na wafuasi wa CUF.
Wakati hayo yakiendelea, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mjini
Magharibi Unguja, kimemfukuza uanachama muasisi wa chama hicho, Hassan
Nassoro Moyo, kwa madai ya kukisaliti chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa, Katibu wa CCM
Mkoa huo kichama, Aziza Iddi Mapuri, alisema chama hicho kimechukua
maamuzi hayo kutokana na muasisi huyo kutoa matamshi yanayokwenda
kinyume cha Chama.
“Mzee Moyo amekuwa akitoa matamshi yanayoashiria chuki na uhasama
kwa wananchi wa Zanzibar na kukisaliti chama hicho, hivyo hafai kuwa
mwanachama,” alisema Mapuri.
Pia alisema Moyo amekuwa akitoa matamshi ya kukisaliti Chama katika
majukwaa ya mikutano ya hadhara inayofanywa na Chama cha Wananchi
(CUF).
“Tarehe 30/4/2014 katika mkutano wa CUF, uliofanyika Kibandamaiti Katibu wa CUF, Seif Sharif Hamad, alimsimamisha mzee
Moyo, ambaye alitamka serikali tatu ndiyo msimamo wa Wazanzibari wote,” alisema Mapuri.
Alisema siyo kweli kuwa msimamo wa Wazanzibari wote ni serikali tatu na kusema kuwa huo ni msimamo wake na wapenzi wake wa CUF.
Mapuri alisema CCM baada ya kutafakari kwa kina imebaini kuwa
kauli na matamshi ya Moyo vimekuwa vikipotosha jamii na wanachama wa
chama hicho na hivyo kupoteza sifa za kuwa mwanachama.
MZEE MOYO ANENA
Moyo kwa upande wake, alisema hajutii uamuzi wa kufukuzwa
uanachama kwa sababu yeye hakuzaliwa kuwa mwanachama wa CCM kwa muda
wote wa maisha yake.
Alisema sababu ya kufukuzwa uanachama iliyotumiwa haina msingi na
kwamba ataendelea kupigania na kutetea maslahi ya Zanzibar hadi mwisho
wa mauti yake.
“Mimi siwezi kurudi nyuma kwa sababu ninachokitetea ni jambo la
haki na ninajua Wazanzibari wengi wapo na mimi katika kuniunga mkono.
Kwa hiyo, kunifukuza hakuwezi kuniziba mdomo,” alisema Moyo kwa njia ya
simu akiwa mkoani Tanga.
Alisema anachotofautiana na CCM ni kuhusu muundo wa Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar na kwamba hakubaliani na Muungano wa serikali
mbili.
Moyo alisema muundo wa serikali mbili upo kwa muda mrefu sasa na
hauna tija kwa wananchi, huku zikiibuka kero za Muungano zisizopata
ufumbuzi wala majibu.
“Mimi ninachoamini ni kuwapo kwa muundo wa Muungano, ambao
utaifanya Zanzibar kuwa na dola yake kamili tofauti na Muungano uliopo
sasa,” alisema Moyo.
Hassan Nassor Moyo kadi yake ya uanachama ni nambari 7 akiwa
miongoni mwa waanzilishi wa CCM iliyozaliwa mwaka 1977 katika Uwanja wa
Amaan na pia ni miongoni mwa viongozi walioshika nafasi za juu katika
Muungano akiwa Waziri wa Katiba na Sheria mwaka 1964.
Katika kipindi kifupi cha miaka ya hivi karibuni, Moyo amekuwa mtu
wa pili kuvuliwa uanachama akitanguliwa na aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo
la Kiembesamaki, Mansor Yussuf Himid.
No comments:
Post a Comment