Arusha.Katika karne ya 15 na 16 , kulikuwa na biashara ya ubadilishaji bidhaa kwa bidhaa. Watu wa jamii moja waliweza kupata mali na bidhaa walizohitaji kwa kubadilishana na jamii nyingine.
Biashara hiyo kwa namna moja au nyingine iliwaumiza watu wa upande mmoja na kuwatajirisha wa upande wa pili.
Mathalan, baadhi ya watu walibadilisha dhahabu kwa
shanga au nguo, wengine wakabadili pembe za ndovu wakati mwingine kwa
pipi na magobole.
Mambo hayo sasa yamebaki historia au simulizi ya
mchana kwani uelewa na mazingira ya wakati huo yalijitosheleza kufanya
hivyo hata bila ya kuhoji.
Hata hivyo, ni jambo la kushangaza kuona hata
katika karne ya 21, bado kuna maeneo ya Tanzania, ambayo watu wake
wanafanya biashara ya kubadilishana bidhaa kwa bidhaa maarufu ‘butter
trade’ licha ya kutambua kuwa wanaumizwa lakini wanakosa njia mbadala wa
kujikwamua.
Ndivyo ilivyo kwa wakazi wa Kijiji cha Shimbumbu,
wilayani Arumeru linapokuja suala la maji. Kwao licha ya kuwa ni
mahitaji ya msingi katika maisha, imekuwa bidhaa adimu na ya thamani
kubwa inayoweza kufananishwa na dhahabu.
Kwa wakazi wa kijiji hicho, maji hugombaniwa na
mwenye nguvu, ndiye atakayepata na wamefikia hatua ya kubadilishana mawe
ya kujengea ili kupata bidhaa hiyo. Hilo linatokea sasa katika karne
hii ya 21.
Licha ya kijiji hicho kuwa kilomita chache kutoka
katikati ya Jiji la Arusha, ambalo lina utajiri wa madini ya Tanzanite
na utalii, wakazi wake wana shida kubwa ya maji.
Kwa haraka, mazingira ya kijiji hicho yanaonyesha
kuwapo uharibifu mkubwa wa mazingira na ukame yanayowaweka wakazi wake
kwenye hali ngumu ya maisha, licha ya ardhi yenye rutuba waliyojaliwa.
Maisha ya Watanzania wa Shimbumbu yanaakisi yale
ya enzi za ujima, huku ikionekana milima ya mawe yaliyochimbwa
yakisubiri malori ya maji yafike ili baishara ya budalishana ifanyike.
Mamia ya ndoo na madumu yaliyo kando ya mawe
yanasubiri ‘kuwa maji’ kwa kubadilishana hali ambayo wakati mwingine
huwa kama sinema kutokana na kugombania.
Jambo hilo linaweza kutajwa kuwa ni aibu
inayotokana na udhaifu wa kimkakati ikiacha maswali mengi yasiyo na
majibu kuhusu binadamu wa Shimbumbu kuishi katika ujima kwenye karne ya
sasa.
Katikati ya kijiji hicho kuna mlima wenye mawe ambayo wananchi hujazana wakiyachimba wakiwa na ndoo za maji wakisubiri wateja.
Swali ni je, mawe yakiisha, wananchi hao wataishije, au utakuwa mwisho wa kunywa maji?
Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Arumeru, Happiness
Mrisho anasema upembuzi ulishafanyika kwa muda mrefu na kiasi cha Sh120
milioni zinatakiwa kumaliza tatizo la maji kwa wakazi wa kijiji hicho.
Mbali na shida hiyo, barabara za eneo hilo
zimeharibiwa kutokana na kubeba mizigo mizito bila ya kufanyiwa
matengenezo na hazifai tena licha ya eneo hilo kuwa na watu wengi.
Diwani wa Kata ya Shimbumbu, Wilson Nyiti anasema
kijiji hicho kina jumla ya wakazi 3,500 wanaotokana na kaya 750 na zote
hazina maji.
Nyiti anasema adha hiyo imesababisha matatizo makubwa kwa wananchi, ikiwamo migogoro ya ndoa, hasa za utotoni.
Anasema mazingira ya kijiji hicho ni mabaya na
hayafai, lakini hakuna jinsi ya kuwazuia wananchi kwani biashara hiyo
ndiyo inayowapa mlo wao na familia kusoma.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana wakati wa ziara yake ya hivi karibuni aliliona hilo.
Katika ziara hiyo, Kinana anaonyesha mshangao na kueleza masikitiko yake kwa eneo hilo kutengwa.
“Hali hii siyo nzuri hata kidogo, barabara mbovu
sijapata kuona, mazingira yameharibika kwa kiasi kikubwa tatizo la Sh120
milioni, ni aibu,” anasema Kinana.
Bila shaka wahusika wataliona tatizo hilo la wana
Shimbumbu na kulifanyia kazi ili kunusuru milima na mazingira ikiwamo
kuwapa nafasi kina mama kufanya shughuli nyingine. Lakini si kijiji
hicho pekee kinachokabiliwa na shida ya maji, bali eneo kubwa la Mkoa wa
Arusha na maeneo mengi nchini.
Machi 16, wananchi wa Arusha walifanya maandamano hadi ofisi za Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (AWSA) wakidai kupata maji.
Maandamano hayo yaliyokuwa ya kushtukiza yalifanyika wakati
maofisa wa AUWSA walipokuwa wakijadili kuhusu maadhimisho ya wiki ya
maji iliyohitimishwa Machi 21.
Tukio hilo lilisababisha Mwenyekiti wa Bodi ya
mamlaka hiyo, Felix Mrema, Mkurugenzi wa AUWSA, Mhandisi Lucy Koye na
wajumbe kukatisha mkutano wao na kukutana na wananchi walioandamana kwa
lengo la kutoa ufafanuzi.
“Maji yaliyopo kwenye chanzo chetu hayatoshelezi
mahitaji ya wananchi, mamlaka inatafuta vyanzo vingine,” alieleza
Mhandisi, Koye.
Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, aliyefika
kwenye tukio hilo alieleza kuwa katika suala hilo hakuna siasa, bali
amekwenda kuungana na wananchi ili kusaidia kutafuta ufumbuzi wa tatizo
la maji akiwataka wananchi kuiwezesha AUWSA kuzalisha maji zaidi kwa
kuondoa vikwazo vilivyopo.
Hata hivyo, takwimu za Serikali zilizotolewa
katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Maji na Waziri wa Maji,
Profesa Jumanne Maghembe mkoani Mara mwezi uliopita zinaonyesha kuwa
zaidi ya wananchi milioni saba wanapata majisafi na salama katika miji
ya mikoa, wilaya na miji midogo nchini kutokana na kuboresha huduma za
majisafi na uondoaji majitaka mijini.
Profesa Maghembe alisemas uboreshaji huo
uliofanyika ni kujenga, kukarabati na kupanua miundombinu ya majisafi
katika miji mikuu ya mikoa, wilaya, miji midogo na miradi ya maji ya
kitaifa.
“Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta
ya Maji imejenga miradi mipya 663 katika vijiji 10 kwa kila halmashauri
nchini na miradi 68 ya upanuzi na ukarabati kupitia Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN).
Utekelezaji huo umekamilisha miradi 731
iliyopangwa kutekelezwa na unajumuisha miradi 390 ambayo haikukamilika
katika mwaka wa fedha 2013/2014,” alisema Profesa Maghembe.
Alisema kuanzia Julai 2013 hadi Desemba 2014,
jumla ya miradi 674 ya maji ilijengwa na kukamilika, idadi ambayo
inachangiwa na ujenzi wa miradi mipya 433 ya vijiji 10 katika kila
halmashauri na miradi mingine 241 ya upanuzi na ukarabati.
“Vijiji 900 vimepatiwa maji na jumla ya vituo
1,8610 vya kuchotea maji vimejengwa ambavyo vinahudumia watu 4,568,402
na kuanzisha vyombo vya watumia maji 560,” alisema na kuongeza.
“Usimamizi huo umeongeza upatikanaji wa huduma ya
majisafi na salama vijijini kutoka asilimia 40 Julai 2013 hadi asilimia
53.08 za sasa.”
No comments:
Post a Comment