Kamanda Kova
Dar es Salaam. Hoja za kisheria alizowasilisha Askofu wa Kanisa
la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusu kutakiwa kuwasilisha nyaraka
10 za utajiri na usajili wa kanisa lake polisi zimezaa matunda.
Sasa, agizo la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam la kumtaka Askofu Gwajima kuwasilisha nyaraka hizo leo
limesitishwa kusubiri utatuzi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
au Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka.
Wakili John Mallya anayemtetea Askofu Gwajima
alilieleza gazeti hili jana usiku kuwa baada ya makubaliano na polisi
mteja wake leo hatafika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam kama ilivyokuwa imepangwa mpaka hoja hizo za kisheria
zitakapotolewa uamuzi.
Alhamisi iliyopita, polisi ilimtaka Gwajima
kuwasilisha vielelezo hivyo, lakini hatua hiyo ilipingwa na kiongozi
huyo akieleza kuwa hatapeleka nyaraka yoyote iwapo jeshi hilo halitajibu
barua aliyoliandikia kutaka liombe vitu hivyo kwa maandishi.
Nyaraka zilizotakiwa kuwasilishwa polisi ni hati
ya usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini
(Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia na nyaraka
za helikopta ya kanisa.
Nyaraka nyingine ni; muundo wa uongozi wa kanisa,
waraka wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za
kanisa, nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama
vya Hiari na kuambatana na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
“Siwezi kuwasilisha kwa mdomo kwa kuwa hizi si
mali za Gwajima… ni mali ya taasisi na si vitu vyake binafsi,” alisema
wakili huyo.
Katika barua yake kwa polisi, Wakili Mallya
alisema: “Tunaiomba Polisi kumwandikia rasmi mteja wetu kimaandishi
nyaraka mnazozihitaji na vifungu vya sheria vinavyotumika na polisi
kutaka nyaraka hizo… tutashukuru kupata hati hiyo.”
Kauli ya Kova
Mapema alipoulizwa kuhusu kitakachotokea leo,
Kamanda Kova alisema: “Suala la Mchungaji Gwajima kwenda na vielelezo
alivyoagizwa na Polisi siwezi kulizungumzia hadi hapo itakapotokea
hakuja navyo ndipo nitakapotoa tamko langu la mwisho.
“Nitazungumziaje hili? Si hadi itokee hakuja na
vielelezo na kama akija navyo halafu mimi nimeongea tofauti, nimeona
italeta malumbano kati yangu na yeye na mimi sitaki ifikie huko.
“Kuna mambo mengi ya kufanya hivyo nitalitolea
tamko la mwisho kwa waandishi wa habari kuhusu mchungaji Gwajima kama
itatokea hivyo ili tuendelee na mambo mengine.”
Mallya alisema nchi inaongozwa kwa sheria, hivyo kila kitu
kinatakiwa kiwe cha kisheria na kwamba wameiandikia polisi kuitaka
waombe nyaraka hizo kimaandishi na kuonyesha vifungu vya sheria
vinavyowaongoza kuziomba badala ya kusema kwa mdomo kwa sababu vitu
hivyo ni vya kanisa na siyo vya Gwajima peke yake.
Askofu Gwajima alihojiwa na Polisi, Kanda ya Dar
es Salaam kwa tuhuma za kumtolea maneno makali Polycarp Kardinali Pengo
baada ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki kutoa tamko lililotofautiana
na la viongozi wa Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu suala la Katiba.
No comments:
Post a Comment