Kinamama wajawazito wanaohudumiwa na kituo cha kusubiri kujifungua cha Chikande manispaa ya Dodoma wameandamana hadi hosipitali ya rufaa ya Dodoma wakilalamikia vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa na walinzi wa hosipitali hiyo ikiwemo kugoma kuwafungulia milango pindi wanapopata uchungu hasa nyakati za usiku na kusababisha baadhi yao kujifungulia njiani.
Kinamama hao zaidi ya 70 wameamua kuchukua uamuzi huo ili kufikisha
kilio chao kwa uongozi wa hosipitali ya rufaa ya Dodoma kufuatia wenzao
wawili hivi karibuni kuzuiwa kuingia hosipitalini hapo na walinzi na
kulazimika kujifungulia kwenye lango kuu la hosipitali na vichakani
hatua ambayo wamedai inawadhalilisha na inahatarisha afya ya mama na
motto.
Kufuatia sakata hilo uongozi wa hosipitali ukalazimika kuitisha
kikao cha dharula na jopo la walinzi wa zamu waliokuwepo kwenye matukio
hayo hali iliyozua malumbano makubwa baina yao huku wakirushiana mpira
kati ya walinzi wa lango kuu na wale wa mlango maalum unaotumiwa na
kinamana hao kuhusu kuhusika na matukio hayo ya unyanyasaji.
Akizungumza kwa niaba ya mganga mfawidhi wa hosipitali hiyo
Dk.Nassoro Mzee muuguzi wa zamu aliyekuwepo wakati sakata hilo linatokea
Cecilia Sanya amesema uongozi wa hosipitali umesikitishwa na kuwepo kwa
matukio hayo na umeahidi kuchukua hatua kwa kampuni ya ulinzi
inayofanya kandarasi ya ulinzi hosipitalini hapo ili kukomesha matukio
ya namna hiyo.
No comments:
Post a Comment