Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia Goran Kopunovic.
Baada ya ushindi wa juzi wa mabao 4-0 dhidi ya Mgambo Shooting kutoka Tanga, Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia Goran Kopunovic, ametangaza vita katika dakika 270 zilizobakia kwa timu yake kuteremka uwanjani kumalizia michezo ya Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.
Mechi ambazo zimebakia kwa Simba ni dhidi ya Ndanda FC kutoka
mkoani Mtwara itakayopigwa Jumamosi Aprili 25, mwaka huu kabla ya Mei 3
kuvaana na mabingwa watetezi, Azam FC huku ikimaliza ligi msimu huu kwa
kuikaribisha JKT Ruvu kutoka Mlandizi mkoani Pwani.
Akizungumza na gazeti hili juzi baada ya mechi dhidi ya Mgambo
Shooting, Kopunovic alisema bado timu yake ina nafasi ya kushiriki
mashindano ya kimataifa mwakani.
Kopunovic alisema mechi zilizobakia kwa timu yake anazifananisha na
'vita' kwa sababu anahitaji kushinda ili aweze kutimiza ndoto ambazo
kwake Mserbia huyo hazijapotea.
"Kimahesabu bado tunaweza kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya
kimataifa, inawezekana, hakuna kukata tamaa mpaka mechi ya mwisho wa
ligi ndiyo tutajua kila kitu," alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya kumaliza mechi ya juzi na kupata ushindi
mnono, sasa anajipanga upya kwa ajili ya kuikabili Ndanda kwa sababu
kila timu inaingia uwanjani kucheza kwa kutumia mbinu tofauti.
"Tumemaliza mechi hii (dhidi ya Mgambo Shooting) sasa tunajipanga
kwa ajili ya Ndanda, ni timu ambayo itakuja na mipango tofauti, ila
tunatarajia kupata ushindani kwa sababu ni moja ya timu ngumu kwenye
ligi hii," aliongeza Kopunovic.
Kocha huyo pia aliwasifia wachezaji wake kwa kuonyesha kiwango cha
juu na kusema kwamba atahakikisha wanaendelea kufanya hivyo kwenye mechi
zilizobakia ambazo zote watacheza kwenye Uwanja wa Taifa.
"Wamenifurahisha sana jinsi walivyocheza, wameonyesha wametumia
akili, na wao wanachezea timu kubwa, nimefurahishwa pia na mchezaji
yosso, Issa (Abdallah) ambaye ametoka Timu B, ana kipaji na atakuwa
tegemeo siku zijazo," alisema Kopunovic.
Simba bado imeendelea kukaa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa
ligi ikiwa na pointi 38 wakati vinara ni Yanga ambao wana pointi 49
huku mabingwa watetezi Azam FC wakiwa na pointi 42.
Timu tatu zinazoshika mkia ni pamoja na Polisi Morogoro, Ndanda
zenye pointi 25 kila moja huku Prisons yenyewe ikiwa na pointi 22.
No comments:
Post a Comment