Tuesday, 21 April 2015

Watanzania 23 waishi kambini Afrika Kusini

Miongoni mwa Watanzania hao, 21 wameridhia kurejea nyumbani na wanatarajia kuwasili nchini muda wowote lakini wengine wawili wameomba kuendelea kubaki huko.
Dar es Salaam. Watanzania 23 wamewekwa kwenye kambi maalumu ya Isipingo nchini Afrika Kusini ili kupewa ulinzi kutokana na mashambulizi yanayofanywa na wazawa wa nchi hiyo dhidi ya wageni.
Miongoni mwa Watanzania hao, 21 wameridhia kurejea nyumbani na wanatarajia kuwasili nchini muda wowote lakini wengine wawili wameomba kuendelea kubaki huko.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema jana kuwa pamoja na maisha ya Watanzania hao kuwa hatarini, hakuna hata mmoja aliyepoteza maisha kutokana na vurugu hizo.
Hata hivyo, alisema kuna Watanzania watatu waliofariki dunia nchini humo kwa sababu nyinginezo.
Membe aliwataja waliofariki kuwa ni Rashid Jumanne ambaye alikuwa jambazi na aliuawa kilomita 90 kutoka Mji wa Durban akiwa kwenye harakati zake za unyang’anyi.
Mtu wa pili alisema ni Athuman China aliyeuawa kwa kuchomwa kisu na wafungwa wenzake ndani ya Gereza la West Hill alikokuwa amefungwa kwa kosa la jinai.
Kijana wa tatu, Ally Mohamed alifariki dunia katika hospitalini alikokuwa amelazwa mjini Johannesburg kutokana na maradhi ya kifua kikuu.
Kijana huyo alifariki baada ya kuugua kwa miezi miwili na tayari mwili wake umewasili nchini kwa maziko.
“Kuna habari zimesambaa mitandaoni kwamba Watanzania wamekufa huko Afrika Kusini. Niweke wazi kuwa hakuna Mtanzania aliyepoteza maisha kutokana na vitendo vya chuki dhidi ya wageni. Mpaka sasa ni watu wanane tu waliopoteza maisha na watu hao wanatoka katika nchi za Ethiopia, Zimbabwe, Malawi na Swaziland.”
Hata hivyo, kuna raia mwingine wa Msumbiji aliyeripotiwa kuuawa.
Membe alisema aliwasiliana na Waziri wa Usalama wa Afrika Kusini, David Mahlobo akamthibitishia kuwa hakuna Mtanzania yeyote aliyeuawa katika vurugu hizo.
Waziri huyo alisema muda wowote Watanzania hao watarudishwa nchini baada ya Serikali ya Afrika Kusini kukubali waondoke.
Alitoa wito kwa Watanzania wote ulimwenguni kujiandikisha katika Balozi za Tanzania huko waliko ili iwe rahisi kuwapata na kuwapa msaada inapotokea hali kama hiyo.
“Hata kama umejilipua, jiandikishe ubalozini ili utambulike uko wapi. Hii itawafanya waweze kupata msaada wa Serikali haraka zaidi,” alisema Membe.
Waziri Membe alisema Watanzania 10,000 wanaishi katika miji ya Durban na Johannesburg lakini hawatambuliki ubalozini.
Hata hivyo, alisema watu wengine wanaosubiri kurudi nyumbani kwa kutegemea mgongo wa Serikali hawatapata fursa hiyo kwani hiyo ni huduma kwa walio hatarini tu.
Wakati huohuo; Chama cha Wananchi (CUF) kimeilaumu Serikali kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka kuwaokoa Watanzania katika vurugu hizo.
Chama hicho kimesikitishwa na mauaji hayo kikisisitiza kuwa wananchi wa Afrika Kusini wamesahau kuwa Afrika ni moja na nchi hizo zilishirikiana katika kupigania ukombozi wa Afrika.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Abdallah Mtolea, imeitaka Serikali ya Afrika Kusini kuongeza nguvu na kukomesha vitendo vya kibaguzi hasa kwa wageni kutoka nje ya Afika Kusini.
“Serikali ya Tanzania haionyeshi kama inawashughulikia Watanzania walioko nchini humo. Tunaitaka Serikali kubeba jukumu la kuwarudisha nyumbani Mara moja Watanzania walioko hatarini nchini humo.”

No comments:

Post a Comment