Rais Jakaya Kikwete.
Wasomi na wananchi mbalimbali, wamemuomba Rais Jakaya Kikwete,
kutosaini Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 huku
wakieleza kuwa kama utasainiwa watahamasisha wananchi kuupinga kwa
kufanya maandamano ya nchi nzima mitaani.
Aidha, wamesema muswada huo ukisainiwa watatumia kama fimbo
kukiadhibu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutokichagua katika uchaguzi
mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Walisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa mdahalo
uliowashirikisha wananchi, wanafunzi mbalimbali wa vyuo vikuu
na wahadhiri wa vyuo vikuu kujadili athari za Sheria ya Takwimu ya
mwaka 2015 na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Wakati wa Bunge la 19 lilohitimishwa Aprili Mosi, mwaka huu,
miswada hiyo iliwasilishwa na serikali bungeni kwa hati ya dharura na
kupitishwa na Bunge na sasa hatua inayofuata utapelekwa kwa Rais kwa
ajili ya kuisaini ili iwe sheria ianze kutumika.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitilia Mkumbo,
akizungumza katika mdahalo huo alisema miswada hiyo kama itasainiwa na
Rais na kuwa sheria, itakuwa na athari kubwa kwa wahadhiri na wanafunzi
wa vyuo vikuu.
Profesa Mkumbo alisema kwa mfano, Sheria ya Takwimu ikianza
kutumika itarudisha nyuma kupata wanafunzi wa PhD kwa sababu masomo yao
yanategemea sana kupata takwimu.
“Usalama mkubwa kuliko wote ni uhuru wa kupata taarifa, kutokupata
taarifa sahihi kuna hatari,” alisema.Profesa Mkumbo alisema Watanzania
wanapenda kulalamika tu vijiweni lakini hawachukui hatua na kwamba
katika suala la muswada huu kuna haja kwa wananchi kuandamana mitaani
ili Rais asisaini. Ndigwa Ezekiel, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, alieleza wasiwasi wake kama suala hilo likienda kupingwa
mahakamani haki itatendeka kwa madai kuwa imeegemea upande wa serikali.
Wachangiaji wengine walisema kama miswada hiyo itasainiwa, hawataipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Wakati wa Mkutano wa Bunge, serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria
ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na kueleza kuwa mtu akatayebainika
kusambaza picha za ngono, miili ya watu waliokufa kwa ajali na
usambazaji taarifa za siri za serikali, atatozwa faini ya Sh. milioni
tano, kifungo kisichopungua miezi sita au vyote kwa pamoja. Hata hivyo,
kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, amesema Rais
Kikwete atatafakari na kuchukua maamuzi sahihi kabla ya
kuusaini Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa mwaka 2015.
Pia amesema Rais Kikwete atasikiliza maoni ya wadau wengine pamoja na kutoa uzito unaostahili kabla ya kusaini muswada huo.
Balozi Sefue aliyasema hayo alipozungumza na NIPASHE kuhusu malalamiko ya wadau ya kumtaka Rais Kikwete kutousaini muswada huo.
Alisema teknolojia ya mitandao inakwenda kwa kasi kuliko udhibiti
wake, hivyo ni lazima kuwapo na usawa katika kudhibiti masuala ya
kimtandao. Balozi Sefue alisema hakuna sheria ambayo itatungwa na
kupendwa na watu wote, lazima kutakuwapo na baadhi ya watu watakaoipenda
na wengine kuikataa.
“Rais lazima atatoa uzito unaostahili kwa muswada unaotoka bungeni. Lakini pia anasikiliza maoni ya watu wengine wanasemaje.
Lakini katika kutoa maamuzi atatoa kwa uzito unaostahili tu,” alisema Balozi Sefue.
Aliongeza: “…sisemi kuwa hatasikiliza maoni ya watu. Lakini
ninachotaka kusema ni kuwa muswada wowote unaotoka bungeni ni lazima
upewe uzito unaostahili…”
Alisema duniani kote, Ulaya na Amerika, wanayo sheria ya kudhibiti
masuala ya mitandao kutokana na kuwapo kwa uhalifu, ambao unailetea
madhara nchi.
Balozi Sefue alisema kila Mtanzania ana uhuru wa kutoa mawazo kwa
kile anachokifikiria, lakini siyo vizuri kutumia lugha ya kumshinikiza
Rais asisaini muswada huo.
Machi 31, mwaka huu, serikali iliwasilisha bungeni Muswada wa
Sheria ya Makosa ya Mtandao, lakini ulipingwa na wadau kwa madai kuwa
hawakushirikishwa na unalenga kudhibiti mawasiliano ya wananchi wenyewe
kwa wenyewe.
Baadhi ya makosa yaliyoainishwa katika sheria hiyo, ni pamoja na
kutuma taarifa bila ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono na za utupu,
udanganyifu unaohusiana na kompyuta, makosa yanayohusiana na utambuzi,
kughushi kunakohusiana na masuala ya kompyuta na kusambaza picha za
utupu za watoto.
Mengine ni unyanyasaji kwa kutumia mtandao, kuchapisha taarifa
yoyote, ambayo itasababisha mauaji ya kimbari, uwongo na matusi ya
kibaguzi, huku adhabu kali ikiwa ni faini ya Sh. milioni 50 au kifungo
kisichopungua miaka saba kwa mtu atakayebainika kusambaza picha za ngono
mtandaoni.
BUNGE
Alipoulizwa kama Bunge limekwishaupeleka muswada huo kwa Rais
Kikwete, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema hawapaswi
kusema kama umepelekwa au la kwa kuwa utaratibu huo ni wa ndani.
“Si utaratibu wetu kusema kama muswada umepelekwa kwa Rais
kusainiwa au la kwa sababu ni utaratibu wa ndani. Hivi ulishawahi
kusikia tumesema jambo kama hilo?” alihoji Dk. Kashililah.
Awali, alipotafutwa Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuhusu suala
hilo alimwelekeza mwandishi kuwasiliana na Dk. Kashililah kwa kuwa yeye
ndiye anahusika zaidi na masuala hayo.
“Mimi niko jimboni, lakini ni vizuri umtafute Katibu wa Bunge kwa
sababu yeye atakuwa anafahamu zaidi na ndiye anashughulikia zaidi mambo
hayo,” alisema Ndugai.
Aliongeza: “ Kwani mna wasisiwasi kwamba, unaweza kukwama? Mimi naamini mpaka Bunge lijalo utakuwa umesainiwa.
Naomba umuulize Katibu wa Bunge ndio atakueleza vizuri kwa kuwa mimi sipo siwezi kufahamu.”
Hivi karibuni makundi mbalimbali, zikiwamo asasi za kiraia,
zilionekana kupinga muswaada huo na kumtaka Rais Kikwete asisaini mpaka
pale sheria hhiyo itakaporudishwa bungeni kuondoa vifungu vinavyokwenda
kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na haki za
binadamu kwa ujumla.
NIPASHE iliona nakala ya barua iliyokuwa imeandikwa na asasi 53 kwenda kwa Rais Kikwete kumtaka asisaini sheria hiyo.
Barua hiyo ilisema sheria hiyo itaminya kwa kiasi kikubwa uhuru wa
wananchi kuwasiliana na kupashana habari endapo itasainiwa bila
marekebisho.
“Ni dhahiri sheria hii imelenga kufuta kabisa uhuru wa mawasiliano
na matumizi ya mitandao ya kijamii kama Facebook, WhatsApp, Jamii
Forums, Twitter, blog… Kupitishwa kwa sheria hii bila kufanyiwa
marekebisho kutasababisha Watanzania wengi kutiwa hatiani bila sababu,
lakini pia kutaondoa kabisa uhuru wa habari nchini,” ilisomeka hivyo.
No comments:
Post a Comment