Edward Lowassa
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameitaka
jumuiya ya albino nchini kuisukuma Serikali ili Rais Jakaya Kikwete
asaini utekelezaji wa hukumu ya kuwanyonga wauaji wa albino.
Kauli ya Lowassa imekuja wiki moja tu baada ya
Rais Kikwete kusema hajapelekewa majina ya watu 16 waliohukumiwa kifo
kutokana na mauaji ya albino kutokana na mlolongo mrefu wa kisheria
uliopo kabla ya kumfikia.
Rais Kikwete alisema hayo wakati wa ibada maalumu
ya kuwekwa wakfu Askofu Liberatus Sangu kuwa Mhashamu Askofu wa Jimbo
Katoliki la Shinyanga.
Hata hivyo, jana Lowassa aliyekuwa mgeni rasmi
katika kampeni ya matembezi kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa
ngozi (albino) yaliyoandaliwa na Klabu za Mbio za Pole ya Temeke na
kushirikisha vikundi mbalimbali vya Dar es Salaam, alisema:
“Ninampongeza Rais Kikwete kutokana na jitihada zake za kukemea mauaji
ya albino. Pia, nimesikia kuna watu sita wametakiwa kunyongwa lakini kwa
maelezo ya Rais hukumu hizo hazijamfikia, hivyo nawaomba mfanye msukumo
ili Rais asaini.”
Kutokana na kukithiri mauaji hayo, Lowassa
aliiomba Serikali kuunda kamati maalumu itakayokuwa ikichunguza mauaji
ya walemavu hao bila kutegemea kamati za mikoa ili kuongeza ufanisi wa
kuilinda jamii hiyo.
Mwanasiasa huyo anayetajwa kutaka kugombea urais
katika Uchaguzi Mkuu ujao, aliuambia umati uliokusanyika katika viwanja
vya TCC Chang’ombe kuwa suala la ulinzi wa albino si la Serikali pekee
bali la wananchi wote.
Mapema Machi mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania
iliwahukumu watu wanne kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na kosa
la kumuua Zawadi Magindu (32) mwenye ulemavu wa ngozi, mkazi wa Kijiji
cha Nyamaruru, Wilaya ya Geita.
Kifungo cha CCM
Awali wakati akitoa hotuba yake Lowassa alisema
kutokana na kifungo alichowekewa na CCM hawezi kuzungumza mambo mengi
kwa sababu yatamletea balaa.
“Kule CCM bado nina kifungo, nikisema mengi
nitaleta balaa,” alisema huku akishangiliwa na kundi la vijana
waliokuwapo uwanjani hapo.
Lowassa yupo kifungoni na makada wengine watano
ambao ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Januari
Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, Mbunge wa Sengerema William Ngeleja, Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika Stephen Wasira na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Aliyekuwa mbunge wa Temeke (CCM), John Kibaso
alisema Lowassa alikubali kuwa mgeni rasmi baada ya kumuomba aridhie
ombi hilo kutokana na mambo yake ya kisiasa yanayomkabili.
“Awali mgeni rasmi ilibidi awe mbunge wa Ilala, Mussa Zungu
lakini ikabidi tumuombe Lowassa aliyetuambia kuwa anaogopa CCM kwa kuwa
haijaruhusu mambo hayo.
Hata hivyo, ndani ya wiki moja mzee wetu alikubali kushiriki nasi kama mlivyomuona,” alisema Kibaso.
Katika maandamano hayo Lowassa aliviongoza vikundi
mbalimbali vya mbio za pole katika matembezi ya haraka kutoka Uwanja wa
Taifa hadi viwanja vya TCC Chang’ombe.
Pia aliongozana na Mbunge wa Temeke (CCM) Abbas Mtemvu, Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan na Zungu.
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye albino Tanzania
(TAS), Ernest Kimaya alisema ukataji wa viungo na kuuawa kwa watu wenye
ualbino umetia doa nchi jambo ambalo linapaswa kukemewa na wadau
mbalimbali.
Alisema mauaji hayo yameongezeka kwa kasi kuanzia
mwaka 2006 ambapo hadi sasa watu wenye ulemavu huo wameuawa 75,
waliojeruhiwa kwa kukatwa viungo ni 35 na makaburi 15 yalifukuliwa na
kuchukuliwa viungo vya mwili.
No comments:
Post a Comment