Zanzibar. Mwanasiasa mkongwe wa Zanzibar Hassan Mussa Takrima
(72) ameionya CCM kuwa itakuwa katika hatari ya kushindwa vibaya kwenye
Uchaguzi Mkuu kama kitasimamisha “mgombea mwepesi, asiye na mvuto na
asiyekubalika kwa wananchi”.
Takriban wanachama 21 wanatajwa kutaka kumrithi
Rais Jakaya Kikwete atakapomaliza muda wake wa vipindi viwili vya miaka
mitano vinavyoruhusiwa kikatiba, na makada sita wanaonekana kuwa na
nguvu zaidi wanatumikia adhabu ya kutogombea uongozi baada ya kubainika
kuanza kampeni mapema.
Wakati CCM ikitafakari jinsi ya kupata mgombea
wake, vyama vinne vya upinzani na vyenye nguvu zaidi, Chadema, CUF, NCCR
Mageuzi na NLD vimekubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa urais na pia
katika ngazi za ubunge na udiwani.
Katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika
nyumbani kwake Kijiji cha Jumbi kuzungumzia miaka 51 ya Muungano,
Takrima, , ambaye aliwahi kuwa naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar,
alisema kutokana na mabadiliko ya hali ya kisiasa yanayoendelea
kujitokeza nchini, CCM inatakiwa kuchagua mgombea imara kama jiwe kwa
kuangalia sifa na uwezo wa kukabiliana na vuguvugu la upinzani kutoka na
mazingira ya ya kisiasa yanayoendelea kujitokeza Tanzania Bara na
Zanzibar.
Hata hivyo, alisema kwamba ni jambo la kushangaza
wakati imebakiwa miezi sita ya kufanyika uchaguzi mkuu, hadi sasa CCM
imeshindwa kuweka hadharani mgombea wake wa urais wa Muungano, Zanzibar
na nafasi nyingine ili wananchi wapate muda wa kutosha kuwachambua sifa
uwezo na uadilifu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka huu.
Alisema yapo mataifa wagombea wa nafasi nyeti kama
hiyo ambayo hujulikana mwaka mmoja kabla ya ya kufanyika kwa Uchaguzi
Mkuu ili kuwapa nafasi wananchi ya kuwachambua pamoja na kuziba nyufa
za kisiasa kama zitatokea wakati wa mchakato wa kupatata mgombea.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip
Mangula alisema juzi kuwa utaratibu huo katika mazingira ya Tanzania
unaweza kuzua malumbano na migongano kwa kuwa baadhi ya wnasiasa
wanatumia fedha zaidi.
Aidha alisema kwamba iwapo CCM itakaribisha
mizengwe katika kupata mgombea wa urais wa Muungano katika vikao vyake,
inaweza kuandika historia mpya ya kisiasa na kutaka haki na usawa
kutumika.
Alieleza kwamba Watanzania bado wana imani kubwa
na CCM pamoja na kasoro mbalimbali zinazojitokeza yakiwemo matatizo ya
ufisadi baada ya kufanikisha kazi kubwa ya kuimarisha amani na umoja wa
kitaifa.
Alieleza kwamba uwezi kujenga nyumba imara bila
ya kuwa na mawe, chokaa na maji na kusisitiza kuwa lazima CCM isimamishe
mtu mwenye msingi wake binafsi wa kisiasa mvuto kwa wapinga kura
pamoja na kuwa mtu anayekubalika kutokana na usafi wake.
Hadi sasa viongozi wanaotajwa kuwania nafasi hiyo
ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, mawaziri wakuu wa zamani Edward Lowassa na
Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi maalum Professa
Mark Mwandosya, Waziri wa Kilimo na Ushirika Stiven Wasira na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe
Wengine ni Professa Anna Tibaijuka, Naibu Waziri
wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, mbunge wa Sengerema Wiliam
Ngeleja, waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi na balozi
Mstaafu Ali Abeid Karume. Kuhusu mikasa ya ufisadi nchini alisema hali
inaendelea kuwa mbaya kutokana na serikali kutowachukulia hatua vigogo
wanaofanya vitendo hivyo na kueleza kuwa kashifa ya kununuliwa mabehewa
machakavu ya treni inatisha na kusikitisha kutokana na sekta ya
usafirishaji kuwa na umuhimu mkubwa kwa wananchi katika kukabiliana na
matatizo ya umasikini.
Alisema kwamba vitendo vya ufisadi vimekuwa kama fasheni
kutokana na vigogo wanaofanya vitendo hivyo wakiwemo watendaji kuendelea
kulindwa na Serikali licha ya kuwa wanahujumu uchumi wa nchi.
Akizungumzia hali ya kisiasa ya visiwani hapa,
Takrima alisema Serikali ya Ummoja wa Kitaifa (SUK) imesaidia kuimarisha
misingi ya amani na umoja wa kitaifa baada ya wananchi kuishi kwa muda
mrefu wakitengana na kususia shughuli za kijamii kama maziko na harusi
kwa sababu za kisiasa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka
1992.
Hata hivyo alisema kwamba kumeanza kujitokeza cheche zinazohatarisha amani na mshikamano.
No comments:
Post a Comment